KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall, amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wake na ari kubwa ya kupambana walioionyesha walipokuwa wakichuana na Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jana.

Azam FC iliweza kushinda mabao 2-1 katika mchezo huo wa mwisho wa kuhitimisha raundi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na kurejea kileleni kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha jumla ya pointi 39, mabao hayo yote yalifungwa na beki wa kulia Shomari Kapombe.

Akizungumza na mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mchezo huo, Hall alisema walijua kutakuwa na ugumu kwenye mchezo huo, pia uwanja huo ni mgumu kwa sababu mipira inadunda na haujatulia huku akidai kuwa ni ngumu timu kucheza soka la kuvutia kutokana na hali hiyo.

“Lazima ubadilishe na kutumia mipira mirefu, unajua Mgambo ni moja timu bora kati ya tatu ziliopo hapa Tanga, wamechukua pointi hapa walipocheza na Yanga, na waliingia kwenye mchezo wetu wakiwa na morali ya kutoka kushinda mabao 5-1 dhidi ya JKT, hivyo iliwapa hali ya kujiamini, hao walikuja na matokeo hayo mazuri na sisi tulikuja huku tukiwa na matokeo mabaya.

“Dakika 15 za kwanza walicheza kwa kujiamini, lakini baada ya kupata bao lao, hiyo ilituamsha sisi na kuonyesha kiwango kizuri na moyo wa kupambana na kupata mabao hayo, nadhani tungepata ushindi mnono zaidi ya huo wa mabao 3-1 au 4-1, Kipre Tchetche alikosa nafasi nzuri mwishoni, Bocco (John) naye alikosa nafasi nzuri na pia Ame Ally, hivyo nina furaha kubwa na kiwango tulichoonyesha,” alisema.

Hall pia alieleza kufurahishwa na rekodi nzuri waliyoinonyesha msimu huu ya kushinda mechi zao zote za ugenini, akidai kuwa hilo ni jambo zuri na limechangiwa na aina ya kikosi bora alichokuwa nacho.

“Tunapointi nyingi sana kwenye mechi zetu za ugenini, unajua Mwadui, Stand United, JKT Ruvu, Ndanda, Majimaji na hii ya hapa, mechi zote ngumu za ugenini tumepata pointi zote na tunafuraha kwa hilo, na hiyo ni kwa sababu tuna aina yetu ya uchezaji kwenye mechi hizo kutokana na aina ya viwanja hivyo.

“Tunatumia wachezaji tofauti na aina tofauti ya uchezaji zaidi ya ile tunayotumia Chamazi na imekuwa ikifanya kazi, unajua tunacheza kwenda mbele moja kwa moja, haraka na tunacheza mipira ya juu kwa sababu uwanja si mzuri, hivyo tuna kikosi boa kabisa cha kuhimili mambo yote hayo,” alisema.

Bocco, Kapombe waacha gumzo Tanga

Mfungaji pekee wa Azam FC jana, Shomari Kapombe, aliyefikisha jumla mabao saba kwenye ligi hiyo pamoja na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, wameacha gumzo jijini Tanga kutokana na majina yao kutajwa sana na wapenzi wa soka mkoani humo.

Mashabiki wa soka mkoani humo waliohudhuria mchezo wa jana mara kwa mara walipogusa mpira wachezaji hao, walisikika wakisema msiwape nafasi watatupiga hao ni hatari, hasa kutokana na kasi waliyoionyesha kwenye mchezo wa jana.

Kitakwimu mchezaji aliyechezewa rafu nyingi jana ni Bocco, ambaye alikuwa akikwatuliwa kila mara alipogusa mpira kutokana na kuwasumbua mno mabeki wa Mgambo JKT, lakini mwamuzi wa kati, Erick Onoka kutoka Arusha alionekana kuziminya baadhi ya rafu hizo kwa kutotoa maamuzi ya kupigwa mpira wa adhabu ndogo.

Azam FC tayari imesharejea jijini Dar es Salaam leo saa 4 asubuhi na kesho saa 9.00 Alasiri itaanza mazoezi rasmi ya kujiandaa na mchezo wa raundi ya tatu wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya moja ya timu kati ya Ashanti United na African Lyon Jumatatu ijayo.