KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, saa 10.30 jioni ya leo itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani kuvaana na wenyeji wao Mgambo JKT katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC itaingia dimbani ikiwa inafukuzia kurejea kileleni kwenye msimamo wa ligi, ushindi wowote utaifanya kufikisha jumla ya pointi 39 na kuizidi Yanga kwa pointi tatu ambayo ipo kileleni hivi sasa ikifikisha pointi 36 sawa na matajiri hao.

Mabingwa hao wapya wa ubingwa wa Kombe la Kagame, wataingia kwenye mchezo huo wakiwa na ari kubwa ya kuzoa pointi tatu ikizingatiwa walilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya African Sports katika mchezo uliopita huku Mgambo JKT ikiichapa JKT Ruvu mabao 5-1.

Azam FC mpaka sasa imeshinda jumla ya mechi 11 na sare tatu bila kupoteza mchezo wowote huku Mgambo JKT ikikamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia pointi 16 baada ya kushinda mechi nne, sare nne na kufungwa mara sita.

Kitakwimu, rekodi inaibeba sana Azam FC kuelekea mchezo huo kwani katika mechi sita za ligi walizocheza tokea Mgambo JKT ipande daraja msimu wa 2012/2013, matajiri hao wameshinda mechi tatu, mbili wakienda sare na wanajeshi hao wakishinda mchezo mmoja.

Katika mechi hizo zote sita jumla ya mabao 10 yamefungwa, Azam FC ikifunga nane kati ya hayo huku Mgambo JKT ikifunga mawili tu na ni mechi mbili tu zilizoisha kwa sare ya bila kufungana zote zikiwa ni za msimu uliopita.

Mbali na rekodi hizo, timu hizo zilichuana katika mchezo wa kirafiki Desemba mwaka jana katika Uwanja wa Mkwakwani na Azam FC ikaibuka kidedea kwa ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Kipre Tchetche kufuatia pande zuri la pacha wake, kiungo Michael Bolou.

Kocha Stewart Hall auzungumzia

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, akizungumzia mchezo wa leo kupitia mtandao wa www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya jana asubuhi, alisema kuwa wamejipanga kushinda ili kuendelea kutoa presha kwa vinara wa ligi hiyo Yanga.

“Tunatakiwa kushinda mchezo kwa kuwa tumepata sare mechi yetu ya mwisho, hivyo tunatakiwa kushinda ili kuipa presha Yanga na tunajua kwamba kuna njia ndefu ya kwenda bado, unajua namaanisha ya kuwa ni michezo 15 hadi na hauwezi kushinda ligi sasa, na hili nililisema wakati tulipokuwa namba moja kuwa tutulie kwa sababu hauwezi kushinda ligi Desemba au Januari bali unashinda ligi Aprili au Mei.

“Hivyo timu inayoongoza Aprili na Mei ndio itakayoshinda ligi na sio Januari, hivyo tunatakiwa kuendelea kufanya mambo kwa uwiano na tunajua kuwa tunatakiwa kuimarisha kiwango chetu,” kauli ya Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, kuelekea mchezo dhidi ya Mgambo JKT kesho.

“Unajua ya kuwa dhidi ya African Sports tulicheza mchezo mzuri na tulikosa nafasi nyingi za kufunga na wakati wakipiga mpira wa adhabu ndogo tulijisahau na hatukufanya usahihi kwenye kuwakaba na tukawapa bao na aliyepiga kichwa alikuwa huru kabisa, hiyo tunatamiliki mpira na tunajua kuwa tunatakiwa kushinda,” alisema.

Hall aliongeza kuwa katika mchezo huo anatarajia kufanya mabadiliko mawili hadi matatu kulinganisha na kikosi kilichocheza dhidi ya African Sports, huku akidai kuwa atawakosa baadhi ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi ambao ni beki Aggrey Morris, Didier Kavumbagu, Allan Wanga, Ramadhan Singano ‘Messi’.

“Pia nitamkosa Khamis Mcha, ambaye alikosa mazoezi takribani wiki mbili baada ya kubakia Zanzibar akishughulikia matatizo ya kifamilia pamoja na Farid (Mussa), ambaye yupo mjini Moshi akimuuguza mama yake mzazi,” alisema.