KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imerejea tena kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Mgambo JKT mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 39 kileleni ikiizidi Yanga pointi tatu yenye pointi 36 katika nafasi ya pili, lakini iko mbele mchezo mmoja ambao watacheza kesho dhidi ya Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Sare au kipigo chochote kwa Yanga kesho kutaifanya kuendelea kusalia katika nafasi ya pili, ambapo ushindi pekee ndio utakaowarejesha kileleni kwenye msimamo.

Shujaa wa Azam FC kwenye mchezo huo alikuwa ni beki wa kulia, Shomari Kapombe, anayecheza pia kama winga katika mfumo wa 3-5-2 unaotumiwa na Kocha Mkuu Stewart Hall, ambaye amefunga mabao yote muhimu ya vinara hao leo.

Timu zote zilianza mchezo huo kwa kasi ya chini dakika 10 za mwanzo zikiwa zinasomana, lakini walikuwa ni Mgambo JKT walioanza kuliona lango la Azam FC dakika 17 kupitia kwa Bolli Shaibu baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza.

Azam FC walitulia zaidi mara baada ya kufungwa bao hilo na kuanza kupeleka mashambulizi makali langoni mwa Mgambo JKT na hatimaye dakika ya 23 ikapata bao la kusawazisha lililofungwa na Kapombe, alimalizia kwa shuti mpira uliotemwa na kipa Said Lubawa kufuatia shuti kali la nahodha John Bocco.

Dakika 14 baadaye alikuwa ni Kapombe tena, aliyeipatia Azam FC bao la ushindi kwa shuti la kiufundi la chini baada ya kupokea pasi safi ya Bocco na kuwazidi ujanja mabeki wawili wa Mgambo JKT kabla ya kumtungua kwa mara nyingine kipa Lubawa.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa mabao hayo, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Mkuu Stewart Hall, kumpumzisha beki Wazir Salum na nafasi yake kuchukuliwa na David Mwantika.

Kama Kapombe angeendelea kuwa mtulivu kipindi cha pili, angeweza kufunga hat-trick katika mchezo huo baada ya kukosa bao dakika ya 78 akiwa ndani ya eneo la 18 kufutia shuti alilopiga kupaa juu la lango la Mgambo JKT,

Azam FC ilionekana kubadilisha mfumo wa uchezaji kipindi cha pili kwa kucheza soka la kulinda mabao waliyopata, mfumo ambao walifanikiwa baada ya dakika 90 kuisha kwa Azam FC kuzoa pointi zote tatu kwa ushindi huo.

Hata hivyo mwamuzi wa mchezo wa leo, Erick Onoka, kutoka Arusha ambaye kitaaluma ni daktari, alionekana wazi kuwabeba wenyeji kwa kushindwa kutoa uamuzi wowote pale wachezaji wa Azam FC walipokuwa wakifanyiwa madhambi ya makusudi na wachezaji wa Mgambo JKT.

Lakini hilo halikuwanyong’onyesha wachezaji wa Azam FC, ambao walipambana kwa kila namna uwanjani hadi kupata pointi hizo tatu leo.

Ushindi huo umezidi kuiongezea rekodi Azam FC, ambayo mpaka sasa imeshinda mechi zake zote tano walizocheza nje ya jiji la Dar es Salaam, walianza kwa kuzichapa timu za Shinyanga, Stand United (2-0) na Mwadui (1-0), ikaibanjua Ndanda ya Mtwara (1-0), ikaipiga Majimaji ya mjini Songea (2-1) kabla ya kuirarua Mgambo JKT leo.

Mechi nyingine waliyoshinda ya ugenini ni dhidi ya JKT Ruvu waliyoifumua mabao 4-2 katika Uwanja wa Karume, ambapo mpaka sasa kwa mujibu wa rekodi Azam FC imecheza na Mgambo JKT jumla ya mechi saba za ligi na kushinda nne, sare zikiwa mbili na wanajeshi hao wakishinda mchezo mmoja.

Azam FC inatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam kesho saa 11.00 Alfajiri, tayari kabisa kwa kuanza maandalizi ya mchezo wa raundi ya tatu wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya moja ya timu kati ya Ashanti United na African Lyon Jumatatu ijayo.

Kikosi Azam FC kilikuwa hivi;

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Wazir Salum/David Mwantika dk 46, Erasto Nyoni, Serge Pascal, Racine Diouf, Jean Mugiraneza, Himid Mao, Salum Abubakar/Frank Domayo dk 82, John Bocco, Ame Ali/Kipre Tchetche dk 76