KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, pamoja na Yanga zipo kwenye vita kali kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Wakati ligi hiyo ikimaliza raundi ya 14 jana, Azam FC imejisanyia jumla ya pointi 36 sawa na Yanga ambayo ipo kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Azam FC mpaka sasa ikiwa imefunga mabao 28 na kufungwa tisa (+19) huku Yanga yenyewe ikitupia 31 na wavu wao kuguswa mara tano sawa na (+26), cha kuvutia zaidi timu zote hizo ndizo pekee ambazo hazijapoteza mchezo wowote hadi sasa katika ligi hiyo.

Azam FC imeachia kiti cha uongozi kwenye msimamo kufuatia sare ya bao 1-1 iliyoipata juzi dhidi ya African Sports, huku Yanga ikipanda juu baada ya kuifunga Ndanda ya Mtwara bao 1-0 jana.

Vita ya timu hizo inatarajia kuendelea tena keshokutwa, pale Azam FC itakapokuwa ikisaka nafasi ya kurejea kileleni kwa kuchuana na wenyeji wao Mgambo JKT ya Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, ambapo ushindi wowote au sare utaifanya kutimiza hilo.

Yanga yenyewe itashuka dimbani Alhamisi hii kuwakabili Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Taifa, nao endapo wakishinda watakuwa wamerejea tena kileleni.

Hivyo kushindwa kupata matokeo mazuri kwa timu yoyote miongoni mwa hizo kutakuwa kumempa mwanya mwenzake kumpita, vilevile itakuwa imetoa nafasi kwa anayefuatia Simba mwenye pointi 30 kuwasogelea zaidi kama yenyewe itapata matokeo bora.

Stewart aichambua mechi Mgambo JKT

Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Mgambo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema amekipanga kikosi chake kufanya vizuri kwenye mchezo huo baada ya sare waliyoipata katika mechi iliyopita.

“Mgambo itakuwa ni mechi ngumu, wamechukua pointi zao nyingi nyumbani, tayari wamechukua pointi dhidi ya Yanga jijini Tanga, hivyo kila kitu kitakuwa kigumu.

“Nitafanya marekebisho kadhaa kwenye kikosi kilichocheza na African Sports na tutakuwa tofauti kabisa, tayari nina timu akilini mwangu itakayocheza dhidi yao, hivyo tunaangalia mbele zaidi kama unataka kutwaa taji la ligi ni lazima uende kwa Mgambo na kufanya kazi yako vizuri,” alisema.

Timu hizo mbili zitakuwa zikipambana kwa mara ya pili ndani ya mwezi na nusu, kwani Desemba mwaka jana zilimenyana katika mchezo wa kirafiki kwenye uwanja huo huo na Azam FC ikaibuka kidedea kwa bao 1-0, lililofungwa na Kipre Tchetche.

Mgambo JKT itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mabao 5-1 katika mechi iliyopita ya ligi dhidi ya JKT Ruvu iliyofanyika ndani ya Uwanja wa Karume.

Azam FC itaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri kuliko timu nyingine yoyote kwenye ligi hiyo ya kushinda mechi zote za mikoani, ikishinda zote nne ilizocheza mpaka sasa kwa kuzichapa Stand United (2-0) na Mwadui (1-0) zote Shinyanga, kabla ya kuzinyuka Ndanda (1-0) mkoani Mtwara na Majimaji (2-1) mjini Songea.