KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC leo saa 1.00 usiku itakuwa na kibarua cha kuendeleza wimbi la ushindi kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) pale itakapoikaribisha African Sports katika Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Azam FC inayoongoza ligi hiyo kwa pointi 35 mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi hiyo ndani ya mechi 13 ilizocheza, ikishinda mechi 11 na kuambulia sare mbili walipocheza na Yanga na Simba, zinazofuatia katika msimamo huo.

Wakati matajiri hao wakiwa kileleni, wapinzani wao African Sports wapo taabani kwa kuchechemea, mpaka sasa wapo mkiani kwenye msimamo wakiwa wamejikusanyia pointi saba tu, kufuatia ushindi wa mechi mbili, sare moja na kufungwa michezo 10

Baada ya kutofanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, wachezaji wa Azam FC wamepania kuwafuta machozi mashabiki wake kwa kuendeleza makali yao katika ligi hiyo ikiwemo kuonyesha kiwango bora kuanzia mchezo wa leo, hatimaye kutimiza malengo ya kutwaa ubingwa msimu huu.

Hata Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, akizungumza na azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya jana asubuhi, alisema kuwa amesharekebisha makosa yote yaliyotokea kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na kuahidi kuwa anatarajia kikosi chake kitaonyesha mchezo mzuri leo na kushinda.

“Sisi hatujalenga chochote juu ya African Sports, sisi tumelenga juu ya kila kitu kuhakikisha tunarudi kwenye kiwango tulichoonyesha kabla, hivyo kila kitu kinahusu kiwango chetu na sio African Sports,” alisema Hall.

Hall amesema kuwa wamefanya mazoezi ya kutosha tokea waliporejea kutoka Zanzibar kwenye michuano hiyo ikiwemo kuwasahihisha kupitia mikanda ya video (DVD) kwa mechi walizocheza huko na kila mchezaji amekubaliana na yaliyotokea na wameahidi kuonyesha mchezo mzuri

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa bila beki wake tegemeo, Aggrey Morris, aliyekwenda kufanyiwa matibabu ya goti lake la mguu wa kulia nchini Afrika Kusini Jumanne iliyopita na anatarajia kurejea nchini kesho baada ya kumaliza zoezi hilo.

Wachezaji wengine watakaokosekana ni washambuliaji Didier Kavmbagu na Allan Wanga, wanaosumbuliwa na majeraha ya enka huku Khamis Mcha akiwa na ruhusa maalumu ya kushughulikia mambo yake binafsi.

Takwimu zinaonyesha kuwa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imekutana mara mbili na African Sports, zote zikiwa ni kupitia mechi za kirafiki walizocheza kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Azam ikishinda wa kwanza bao 1-0 huku wa pili uliofanyika Desemba mwaka jana ukiisha kwa sare ya bao 1-1.

Ushindi wowote wa Azam FC leo utaifanya iwe imeshinda mechi yake ya nne mfululizo na mchezo wa 12 tokea ligi hiyo ianze, ikiwa pia na rekodi ya ushindi asilimia 100 katika mechi za ugenini walizocheza mikoani na Uwanja wake wa Azam Complex.