TIMU ya vijana ya Azam FC ‘Azam FC Academy’ imezidi kufanya kweli baada ya jioni hii kutoa dozi kali  ya mabao 6-0 kwa vijana wenzao wanaojiita African Sports.

Mchezo huo unaotambuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ulikuwa ni maalumu kwa timu hizo za vijana kucheza kabla ya kuanza mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baina ya timu kubwa ya Azam FC itakaowakaribisha African Sports ya Tanga saa 1 usiku wa leo.

Mabao ya Azam FC Academy leo yametiwa wavuni na mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Shaaban Idd aliyefunga bao moja sawa na Rajabu Odasi huku Yahaya Zaidi na Optatus Lupekenya wakipiga mawili kila mmoja.

Timu hiyo ilionekana kutakata zaidi kipindi cha pili mara baada ya kusikiliza mawaidha ya makocha wao, na ilishuhudiwa mabao hayo yakiingia kama mvua kuelekea mwishoni mwa kipindi cha pili na kama wachezaji wa Azam FC Academy wangekuwa makini zaidi wangeweza kupata ushindi mnono zaidi.  

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwenye mechi ya pili ya mwaka huu kwa timu hiyo ndani ya wiki hii, kwani Alhamisi iliyopita waliichapa timu ya jeshi ya Green Warriors bao 1-0, lililofungwa na Alphonce Lukani.  

Azam FC Academy inanolewa na Kocha Mwingereza, Tom Legg, anayesaidiana na mzawa, Idd Cheche, aliyevumbua vipaji vingi hadi sasa ndani ya academy hiyo.