KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho mchana kujipanga na mechi zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) mara baada ya kutoka katika michuano ya Kombe la Mapinduzi jioni ya leo.

Azam FC imeaga michuano hiyo mara baada ya kupoteza mchezo wa mwisho wa Kundi B kwa kufungwa na Mafunzo mabao 2-1, uliofanyika Uwanja wa Amaan visiwani hapa.

Vinara hao wa ligi wenye pointi 35, ndio walioanza kufumania nyavu za Mafunzo kupitia Kipre Tchetche, aliyefunga bao safi la kichwa akimalizia kona iliyochongwa na beki wa kulia Shomari Kapombe.

Azam FC ingeweza kujipatia mabao zaidi kipindi cha kwanza kama washambuliaji wake Tchetche na Allan Wanga wangekuwa makini kuzitumia nafasi kadhaa walizopata kabla ya kupatikana bao hilo la uongozi.

Dakika ya 35, Mafunzo ikapata bao la kusawazisha lililofungwa na Rashid Abdallah aliyeuwahi mpira uliokuwa ukitoka nje kufuatia krosi ya Ally Hassan.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu zote zilienda mapumziko zikiwa nguvu sawa, ambapo Azam FC ilianza kipindi cha pili kwa kasi kubwa ikitaka kupata mabao zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu nusu fainali.

Lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda wachezaji walionekana kuchoka, hiyo iliwafanya Mafunzo kuandika bao la pili kupitia kwa Sadick Habib dakika ya 90, aliyemalizia mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Haji Abdi.

Kuchoka kwa wachezaji wa Azam FC kwa kiasi fulani kumechangiwa na kucheza mechi nyingi ndani ya muda mchache, wakicheza mechi tano za kubwa za kiushindani ndani ya siku 12 kuanzia Desemba 27 mwaka huu walipocheza mechi ya ligi dhidi ya Kagera Sugar hadi leo Januari 7 walipochuana na Mafunzo.

Mechi nyingine walizocheza katikati ni dhidi ya Mtibwa Sugar Desemba 30 kabla ya kuanza mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar na siku moja baadaye ikacheza mechi ya pili dhidi ya Yanga kabla ya kumaliza na Mafunzo.

Azam FC itaanza safari yake ya kurejea Dar es Salaam kesho saa 6 mchana kwa usafiri wa boti, itarejea ikiwa kamili tayari kabisa kujiimarisha na kujidhatiti kubakia kileleni kwenye msimamo wa ligi na kuivuatia kasi michuano ya Kombe la FA watakaloanza kukipiga na Ashanti United Januari 26 pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa:

Ivo Mapunda, Shomary Kapombe/Khamis Mcha dk 79, Erasto Nyoni, Serge Wawa, Abdallah Kheri, Farid Mussa/Ramadhani Singano dk 65, Salum Abubakar, Mudathir Yahaya/Frank Domayo dk 65, Allan Wanga, Michael Bolou/Ame Ali dk 69 na Kipre Tchetche.

Mafunzo; Khalid Mahadhi, Juma Mmanga/Kheri Salum dk 10, Haji Mwambe, Haji Hassan, Said Shaaban, Ali Hassan/Jermaine Seif dk 58, Samih Nuhu/Ahmed Maulid dk 84, Hassan Juma, Abdulaziz Makame, Rashid Abdallah na Shaaban Ali/Sadick Habib dk 72.