TIMU ya Azam FC imeanza kampeni ya kuwania taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar, mchezo uliofanyika usiku wa kuamkia leo kwemye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alikifanyia marekebisho makubwa kikosi chake tofauti na kile kilichocheza mara ya kwanza na Mtibwa Sugar Jumatano iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na kuisha Azam kushinda kwa bao 1-0.

Katika eneo la ulinzi aliwapumzisha kipa Aishi Manula, mabeki Pascal Wawa, Racine Diouf na Racine Diouf na kuwaanzisha Mwadini Ali, Said Morad, David Mwantika na Gardiel Michael.

Wengine wapya walioanza leo ni Ramadhan Singano ‘Messi’, Khamis Mcha ‘Vialli’, Mudathir Yahya, Himid Mao ‘Ninja’ na washambuliaji Allan Wanga na Ame Ally.

Azam FC ilianza vema mchezo huo kwa kuanza kulishambulia kwa kasi lango la Mtibwa Sugar, lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda wapinzani wao walionekana kuimarika na kumiliki mchezo.

Hivyo hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zimalizika timu hizo zilikuwa bado hazifungana, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko mawili kwa kutoka Khamis Mcha, Ame Ally na kuingia Frank Domayo na Kipre Tchetche.

Mabadiliko hayo yaliiimarisha Azam FC, ambayo ilianza kupeleka mashambulizi ya kasi langoni mwa Mtibwa Sugar, dakika 53 Tchetche alikosa bao la wazi baada ya kupiga kichwa kilichopaa juu ya lango akimalizia krosi safi ya Gardiel.

Messi aliyekuwa akiwapa shida mabeki wa Mtibwa Sugar, naye alifanya shambulizi kali langoni mwa Mtibwa Sugar kwa kuwatoka mabeki wao watatu kabla ya kipa Said Mohamed kumvamia na kuokoa hatari hiyo na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Mtibwa Sugar ilipata bao la kuongoza dakika ya 60 kupitia kwa Hussein Javu aliyepiga shuti baada ya kupewa pasi na Shizza Kichuya, aliyepokea mpira kutoka kwa beki wa Azam FC, Said Morad aliyefanya uzembe ndani ya eneo la 18.

Kocha Hall alifanya mabadiliko mengine dakika ya 71 kwa kuwatoa Wanga, Mao, Gardiel na kuwaingiza John Bocco, Wazir Salum na Jean Mugiraneza.

Haikupita dakika mbili, nahodha Bocco akaisawazishia Azam FC bao hilo kwa njia ya mkwaju wa penalti kufuatia kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mabeki wa Mtibwa Sugar.

Hadi dakika 90 za mchezo huo zinamalizika timu hizo ziligawana pointi kufuatia sare hiyo, zote zikiwa na pointi moja kwenye Kundi B.

Kinara wa kundi hilo ni Yanga iliyoanza kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar.

Azam FC itashuka tena dimbani kesho saa 2.15 usiku kuvaana na Yanga, mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi:

Mwadini Ali, Ramadhan Singano, Gardiel Michael/Wazir Salum dk 71, Abdallah Kheri, Said Morad, David Mwantika, Himid Mao/Jean Mugiraneza dk 71, Mudathir Yahya, Khamis Mcha/Frank Domayo dk 45, Allan Wanga/John Bocco dk 71, Ame Ally/Kipre Tchetche dk 45