KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho saa 2.15 usiku inatarajia kuanza kampeni ya kuwania ubingwa wa michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuvaana na Mtibwa Sugar.

Mchezo huo wa Kundi B utafanyika katika Uwanja wa Amaan visiwani hapa Zanzibar, ukitanguliwa na mechi nyingine ya kundi hilo utakaowakutanisha Yanga watakaocheza na  Mafunzo ya Zanzibar utakaoanza saa 10.30 jioni.

Timu hizo zinakutana ikiwa ni siku nne tu zimepita tokea wapambane kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) katika mchezo mkali na mgumu uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Katika mchezo huo, Azam FC iliibuka kidedea kwa kushinda bao 1-0, lililofungwa kiufundi kwa faulo ya moja kwa moja na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ dakika ya 87 na kuifanya timu hiyo kurejea kileleni baada ya kufikisha jumla ya pointi 35.

Mara ya mwisho Azam FC kucheza na Mtibwa Sugar kwenye michuano hiyo ilikuwa ni Januari 8, mwaka jana katika hatua ya robo fainali, Mtibwa ilienda hatua ya nusu fainali kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 7-6 kufuatia dakika 90 kuisha kwa sare ya bao 1-1.

Hivyo mchezo huo utakuwa ni wa kisasi kwa pande zote mbili, Azam FC ikitaka kulipa kisasi cha mwaka jana huku Mtibwa Sugar yenyewe ikitaka kusawazisha makosa ya kupoteza mechi ya ligi dhidi yao Jumatano iliyopita.

Azam FC leo asubuhi ilifanya mazoezi ya kwanza visiwani Zanzibar mara baada ya kuwasili jana jioni tayari kabisa kwa kusaka pointi tatu muhimu dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kocha Mario ataja mipango

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Mario Marinica raia wa Romania, ametabiri tena ugumu kwenye mchezo huo huku akiweka bayana kuwa kikubwa walicholenga ni kuendeleza ubora wao.

“Hii ni changamoto nyingine kwetu kwenye michuano hii mipya tunashiriki, itakuwa ni mechi ngumu. Lakini kitu cha kwanza tumeweza kutengeneza kiwango bora kwa kila mchezaji wetu pamoja na timu nzima kwa ujumla.

“Tumetwaa ubingwa wa Kagame, tunaongoza ligi hivi sasa, hivyo kupitia michuano hiyo tunatakiwa kuhakikisha tunaendeleza ubora wetu, tuliojijengea wenyewe mpaka sasa, tuna kikosi kizuri na tutaitumia michuano hiyo kubadilisha kikosi mara kwa mara kwa kila mchezaji aliyekuja hapa kupata nafasi ya kucheza,” alisema.

Marinica alisema kuwa wapinzani wao hao ni timu nzuri akidai kuwa ina safu bora ya ulinzi na ushambuliaji kulingana na takwimu zao hivi sasa, jambo ambalo limewafanya kushika nafasi ya tatu kwenye ligi mpaka sasa.

“Tunatarajia kufanya marekebisho kwenye kikosi kitakachocheza kesho pamoja na mfumo wa uchezaji uwanjani, siwezi kusema kwa sasa, nadhani kila mmoja atajionea kesho,” alisema.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB imelitwaa taji hilo mara mbili chini ya Kocha Stewart Hall, aliyerejea tena tokea Mei mwaka jana kuinoa timu hiyo kwa mara ya tatu, mara ya mwisho kulibeba ilikuwa ni mwaka 2013 walipoifunga Tusker ya Kenya mabao 2-1.