KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam leo saa 9 alasiri kwa usafiri wa boti kuelekea visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Azam FC imepania kulitwaa tena taji hilo mwaka huu baada ya kulikosa tokea 2013, walipolitwaa mara ya mwisho kwa kuifunga Tusker ya Kenya mabao 2-1.

Tayari Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, aliyetwaa kombe hilo mara mbili ameshaweka wazi kuwa ataitumia michuano hiyo inayoanza kesho kuwapa nafasi zaidi wale wachezaji ambao hawakupata nafasi ya kucheza muda mwingi kwenye mechi za ligi.

Mchezaji pekee wa Azam FC ambaye ataikosa safari hiyo ni winga Farid Mussa, anayekwenda kwenye majaribio ya siku 10 kwa mabingwa wa Slovenia, FC Olimpija Ljubljana.

Farid ataondoka nchini mapema wiki ijayo kuungana na timu hiyo nchini Hispania kwa ajili ya majaribio hayo.

Beki kisiki Aggrey Morris, naye atakosekana kutokana na kuuguza majeraha ya goti yanayomsumbua (meniscus).

Azam FC itaanza kutupa karata yake ya kwanza keshokutwa Jumapili kwa kucheza na Mtibwa Sugar, waliopangwa nao Kundi B sambamba na timu nyingine za Yanga na Mafunzo ya Zanzibar.

Mchezo wa pili itaumana na Yanga Jumanne ijayo, mechi hizo zote zikiwa ni saa 2.15 usiku na itafunga dimba kwa hatua ya makundi kwa kuvaana na Mafunzo ya Zanzibar Alhamisi ijayo saa 10.30 jioni.

Mabingwa hao wa Kombe la Kagame, wanaelekea kwenye michuano hiyo wakiwa wametoka kufanya vizuri katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu, mpaka sasa wakiwa kileleni kwa kujikusanyia jumla ya pointi 35 kati ya 39 ndani ya mechi 13 ilizocheza.