KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imerejea rasmi kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex jioni ya leo.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 35 baada ya kushinda mechi 11 na sare mbili huku ikiiacha Yanga iliyoangukia nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia pointi 33.

Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua na kasi muda wote, ulianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, lakini Azam FC itajilaumua yenyewe baada ya kupoteza nafasi za kufunga mabao kupitia kwa nahodha John Bocco, Shomari Kapombe na Jean Mugiraneza ndani ya dakika 30 za mwanzo.

Mtibwa Sugar ilitumia kipindi cha kwanza kwa kucheza kwa kasi na kuwabana viungo wa Azam FC wakiwazuia wasiwalishe mipira ya hatari washambuliaji walioanzishwa leo Bocco na Didier Kavumbagu.

Hadi filimbi ya mwamuzi Ngole Mwangole kutoka Mbeya inapulizwa kuashiria kumalizika kwa kipindi cha kwanza, timu zote zilienda vyumbani kusikiliza mawaidha ya makocha wao zikiwa bado suluhu.

Azam FC ilirejea mchezoni kwa kushindo mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya mabadiliko ya kuingia kwa wachezaji watatu Ramdhan Singano ‘Messi’, Mudathir Yahya na Kipre Tchetche na kutoka Didier Kavumbagu, Farid Mussa na Frank Domayo.

Kasi ya Tchetche, Messi na ushirikiano bora wa viungo Mudathir, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Mugiraneza, ulipunguza kwa kiasi kikubwa mashambulizi ya Mtibwa Sugar na Azam FC ilionekana kuwa na kiu ya kusaka bao la ushindi.

Juhudi za Azam FC zilizaa matunda dakika ya 87 baada ya nahodha John Bocco kufunga bao safi la mpira wa adhabu ndogo alioukata kwa chini na kuwapita mabeki wa Mtibwa Sugar na kipa wa timu hiyo, Said Mohamed, kabla ya kujaa wavuni.

Faulo hiyo iliyokuwa nje kidogo ya eneo la penalti (edge), ilitokana na beki wa Mtibwa Sugar Salim Mbonde kumfanyia madhambi ya makusudi kwa kumvuta chini mfungaji wa bao hilo, Bocco.

Bao la Bocco liliwainua vitini mashabiki wa Azam FC, walioshangilia kwa nguvu kubwa huku wachezaji wakikimbilia kwenye benchi la ufundi kwenda kushangilia na wachezaji waliokuwa benchi pamoja na benchi zima la ufundi.

Pia bao hilo lilizima kelele za mashabiki wa Yanga na Simba, waliojazana kwa wingi kwenye uwanja huo kuwazomea wachezaji wa Azam FC ili wasipate matokeo mazuri na kuwashangilia wapinzani wao katika mchezo huo, lakini hadi dakika 90 zinamalizika waliondoka uwanjani wakiwa vichwa chini.

Bocco anakuwa amefikisha bao la sita kwenye ligi msimu huu akikaribiana na Tchetche aliyefunga saba, huku akiwa na kibarua cha kufunga mabao mengine manne ili amfikie kinara wa mabao Amissi Tambwe (Yanga) aliyetupia 10 mpaka sasa.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa mabadiliko aliyofanya kipindi cha pili kwa kiasi kikubwa yaliwafanya warejee mchezoni baada ya kupwaya kipindi cha kwanza.

“Kuingia kwa Messi, Mudathir kulifanya tucheze vizuri sana kwenye sehemu ya kiungo, wote wakisaidiana vizuri na Sure Boy. Kipindi cha kwanza hatukuwa vizuri, Mtibwa ilitunyima nafasi ya kucheza,” alisema.

Hall alisema kuwa anafuraha kubwa kuiongoza Azam FC kumaliza mwaka 2015 wakiwa kileleni kwenye msimamo wa ligi na kudai kuwa ni dalili nzuri kwao ya kutwaa ubingwa huku akisisitiza ni lazima wafanye kazi kubwa kufikia mafanikio hayo.

“Hivi sasa tunaenda kwenye Mapinduzi Cup, nitaitumia michuano hiyo kuwaweka fiti wachezaji wangu, wale wachezaji ambao hawakupata nafasi nitawapa kipaumbele, nadhani itakuwa ni michuano mizuri itakayotujenga kwa ajili ya kuja kumalizia mechi za ligi zilizobakia,” alisema.

Azam FC na Mtibwa Sugar zitakutana tena Jumapili hii kwenye mchezo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi wote wakiwa wamepangwa Kundi B sambamba na timu nyingine za Yanga na Mafunzo ya Zanzibar.

Kikosi cha Azam FC kilichocheza:

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Abdallah Kheri, Racine Diouf, Pascal Wawa, Jean Mugiraneza, Frank Domayo/Mudathir Yahya dk62, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco, Didier Kavumbagu/Kipre Tchetche dk62 na Farid Mussa/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk55.

Mtibwa Sugar: Said Mohammed, Ally Shomari, Issa Rashid, Salim Mbonde, Andrew Vicent, Henry Joseph, Said Bahanuzi/Jaffar Salum dk60, Mzamiro Yassin, Boniface Maganga, Mohammed Ibrahim/Ibrahim Rajab dk82 na Shizza Kichuya.