KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, saa 10.00 jioni ya leo itakuwa kibaruani kuvaana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikijikusanyia pointi 29 baada ya kushinda mechi tisa, sare mbili na haijafungwa hata moja, ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Majimaji katika mchezo uliopita.

Kagera Sugar wenyewe wapo nafasi ya 15 kwenye msimamo wakiwa na pointi tisa baada ya kufungwa mechi saba, sare tatu na wiki iliyopita walipata ushindi wao pili msimu huu kwa kuifunga African Sports ya Tanga bao 1-0.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema maandalizi yote waliyofanya kwa ajili ya mchezo huo yameenda vizuri na kudai kuwa haitakuwa mechi rahisi kama wengi wanavyodhania.

“Maandalizi yetu yameenda vizuri na nashukuru Mungu wachezaji walipata muda wa kupumzika jana (juzi), walikuwa pamoja kwenye sikukuu ya Krismasi, hili ni jambo zuri katika kuongeza morali ya wachezaji na kuwapa moyo.

“Hautakuwa mchezo rahisi kwani Kagera ipo nafasi mbaya kwenye msimamo wa ligi, wapo chini na hii imechangiwa na wao kutokuwa na uwanja, unajua wanatengeneza uwanja wao kwa sasa, hivyo kila mchezo waliocheza mpaka sasa wamecheza ugenini,” alisema Hall.

Kocha huyo aliyeipa Azam FC kombe la kwanza la ubingwa wa Kagame Agosti mwaka huu, alisema kuwa jambo kubwa timu yake watakalofanya ni kupambana, kufanya kazi kwa nguvu uwanjani, kucheza kiprofesheno ili kupata ushindi.

“Kagera wanaweza kuwa hatari kwetu, hatuwezi kuchukulia mechi kirahisi kutokana na nafasi waliyopo, hivyo tutafanya mambo kiprefesheno kama tulivyofanya dhidi ya Majimaji,” alisema.

Hall aliongeza kuwa katika mechi ya leo anatarajia kubadilisha mfumo wa uchezaji kwa nyakati tofauti ili kukabiliana na upinzani kutoka kwa timu hiyo na hata nyingine zitakazokuja mbeleni, akitumia mifumo ya 3-5-2 na 3-4-3.

Mabingwa hao wa ligi hiyo msimu wa 2013/14 walipolitwaa bila kufungwa mchezo wowote, wataendelea kukosa huduma ya beki kisiki wa kati Aggrey Morris aliye majeruhi, ambaye atakoseka katika mchezo wa tatu mfululizo.

Azam FC ikishinda mchezo huo itakuwa imepunguza pengo la pointi dhidi yake na Yanga inayoongoza kileleni kwa 33, lakini wakiwa wamecheza michezo miwili mbele zaidi ya matajiri hao.

Hivyo Azam FC ikipata pointi tatu leo na kushinda tena katika mchezo wake mwingine dhidi ya Mtibwa Sugar Jumatano ijayo, itakuwa imerejea rasmi kwenye nafasi yake ya awali kileleni kwa kuiteremesha Yanga.