KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendeleza kasi yake ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) baada ya kuwachapa Kagera Sugar mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex jioni ya leo.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alifanya mabadiliko ya wachezaji wanne katika kikosi kilichoanza leo, akiwaanzisha beki Racine Diouf, kiungo Himid Mao, Michael Bolou na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao hawakucheza mchezo uliopita dhidi ya Majimaji.

Azam FC ilianza vema pambano hilo na kujipatia bao la mapema dakika ya 9 lililofungwa kwa kichwa na mshambuliaji hatari kutoka Ivory Coast, Kipre Tchetche, akimalizia kona safi iliyochongwa na kiungo Himid Mao ‘Ninja’.

Bao hilo limemfanya Tchetche kufikisha bao la saba kwenye ligi msimu huu, akizidiwa mabao matatu na anayeongoza kileleni Amissi Tambwe (Yanga) aliyefunga 10.

Kagera Sugar iliamka mara baada ya kufungwa bao hilo na walijitahidi kuziba mianya ya hatari langoni mwao kwa kumiliki mpira muda wote, jambo ambalo liliwafanya washambuliaji wa Azam FC kushindwa kupata mipira.

Azam FC ilipata pigo dakika ya 34 baada ya kuumia misuli ya paja kwa beki Erasto Nyoni, aliyekuwa akicheza beki wa kati upande wa kulia, ambaye alipumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Kheri ‘Sebo’.

Haikupita dakika, mwamuzi wa mchezo wa leo Selemani Kinugani kutoka Morogoro, akaipatia penalti Kagera Sugar, akidai kuwa beki wa Azam FC Racine Diouf alimfanyia madhambi mshambuliaji Ramadhan Kipalamoto.

Lakini umahiri wa kipa wa Azam FC, Aishi Manula, uliweza kuinyima bao Kagera Sugar baada ya kuiokoa penalti hiyo kwa mguu wake iliyopigwa na beki wa timu hiyo, Salum Kanoni.

Aishi anakuwa amedaka penalti ya tatu kwenye msimu huu wa ligi, ya kwanza akianza kumdakia Rashid Mandawa wakati Azam FC ilipoichapa Mwadui bao 1-0 huku nyingine akimdakia kiungo wa Yanga, Thabani Kamusoko kwenye sare ya bao 1-1.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa bao hilo, ambapo kipindi cha pili kilianza kwa Stewart Hall kumpumzisha nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Maliki.

Kama mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbagu, angekuwa makini angeweza kuifungia mabao mawili timu hiyo, lakini alishindwa baada ya kupoteza nafasi hizo za wazi akiwa kwenye eneo la mita sita la kipa.

Wakati Kagera Sugar ikiwaza kupata bao la kusawazisha kwa kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Azam FC, ilijikuta ikipigwa bao la pili lililofungwa kiustadi na beki Shomari Kapombe, aliyeitumia vema pasi safi aliyopewa na kiungo machachari Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Bao hilo liliwamaliza kabisa Kagera Sugar waliopoteza nafasi nyingi za wazi, na kupelekea dakika 90 za mchezo huo kuisha kwa ushindi huo wa Azam FC na mabao mawili ya kufunga.

Ushindi huo umeifanya Azam FC kuisogelea nafasi yake ya kileleni mwa msimamo wakifikisha pointi 32 katika nafasi ya pili, lakini inazidiwa mchezo mmoja wa kucheza na Yanga inayoongoza kwa pointi 33

Hivyo ushindi wowote wa Azam FC kwenye mchezo wake wa kiporo dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaofanyika Jumatano ijayo utaifanya kurejea kileleni katika msimamo kwa kufikisha jumla ya pointi 35.

Akizungumza kwa ufupi na mtandao wa azamfc.co.tz, mara baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa timu yake haikucheza vema kipindi cha kwanza kutokana na kujaribu mfumo mpya wa 3-4-3, ambao ulishindwa kufanya kazi kama alivyopanga.

“Mchezo ulikuwa mgumu, nadhani hatukucheza vema kipindi cha kwanza kutokana na mfumo mpya tuliotumia, washambuliaji watatu niliowatumia walishindwa kupata mipira badala yake mipira mingi ilienda kwa Kapombe japo tulipata bao moja kipindi hicho, kipindi cha pili tulirejea kwenye mfumo wetu wa 3-5-2, tuliinuka kidogo,” alisema.

Hall alisema anajaribu kubadilisha mfumo wa uchezaji kutokana na timu nyingi kuuzoea mfumo wa awali wa 3-5-2 waliokuwa wakiutumia, ambao umewapa ubingwa wa Kombe la Kagame kwa kishindo wakilitwaa bila kuruhusu wavu kuguswa na bila kufungwa mchezo wowote.

Mwingereza huyo, pia aliuzungumzia mchezo ujao dhidi ya Mtibw Sugar, akitabiri kuwa utakuwa mgumu sana kama aliokutana nao kwa Kagera Sugar na kudai kuwa alimpumzisha nahodha John Bocco kipindi cha pili leo ili awe vizuri zaidi kwa mchezo huo.

“Tuna siku chache sana za maandalizi kabla hatujaingia kwenye mchezo huo, hivyo ndio maana nimempuzisha Bocco, kwa kuwa amecheza dakika 90 kwenye mechi mbili zilizopita (Simba, Majimaji), nataka awe vizuri kwenye mchezo huo.

“Mara moja tutaanza maandalizi kwa mchezo huo, kesho jioni wachezaji waliocheza leo watapata fursa ya kurudisha miili yao vizuri kwa kuogelea na kukaa kwenye mapipa ya maji yenye mabarafu, wale ambao hawakucheza nitakuwa nao pamoja katika mazoezi ya nguvu ya kuwaweka fiti,” alisema.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa;  

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni/Abdallah Kheri dk34, Serge Wawa, Kipre Bolou/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk 68, Racine Diouf, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Himid Mao, Kipre Tchetche, John Bocco/Farid Mussa dk46 na Didier Kavumbangu.

Kagera Sugar: Anthony Agaton, Salum Kanoni, Juma Jabu, Erick Kyaruzi, Shaban Ibrahim, Mbaraka Yusuph, Daud Jumanne, Martim Lupart, Ramadham Kipalamoto na Paul Ngwai/Adam Kingwande dk58.