TIMU ya Azam FC Academy jana ilifanya mauaji makubwa kwenye soka baada ya kuwachapa vijana wenzao wa Kingunge Superstar mabao 32-0 kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.

Azam FC Academy ilianza mchezo huo kwa kasi kubwa, jambo ambalo liliwafanya vijana kutoka na ushindi mnono kipindi cha kwanza kwa kuongoza kwa jumla ya mabao 16-0.

Miongoni mwa mabao hayo, mshambuliaji hatari wa timu hiyo Shaabani Iddi alifunga matano sawa na Optatus Lupekenya, Joshua John alifunga mawili huku Charles Stanslaus, Yohana Mkomola, Abdul Omar na Said Issa wakifunga bao moja kila mmoja.

Kipindi cha pili kilianza tena vizuri kwa upande wa kikosi cha Azam FC Academy, ambacho kilifanyiwa mabadiliko mengi, jambo lililopelekea kupata karamu nyingine ya mabao, wakifunga 16, safari hii Sadallah Mohamed aliibuka kinara kwa kufunga matano peke yake.

Wengine waliofunga kipindi cha pili ni Yahaya na Rajabu Odas, ambao kila mmoja alifunga mabao matatu, Masoud Abdallah alitupia mawili huku Alfons Mkani, Abas Kapombe na Stanslaus Ladiscaus wakiongeza bao moja kila mmoja.  

Ushindi huo wa Azam FC Academy unaifanya kuvunja rekodi yao wenyewe waliyoiweka mwanzoni mwa mwaka huu kwa kuichapa timu ya Chuo cha Biashara cha CBE mabao 31-0.

Azam FC Academy ni kituo namba moja cha kukuza vipaji nchini kilichotoa na kukuza nyota kadhaa wanaotamba kwa sasa nchini wakiwemo viungo hatari kwa sasa nchini Himid Mao na Mudathir Yahya, kipa Aishi Manula, mabeki Abdallah Kheri, Gardiel Michael.

Kingunge Superstar ni academy iliyoanzishwa hivi karibuni maeneo ya Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam, ikiwa imefanya vizuri kwa kuzifunga timu nyingi zilizo karibu na eneo hilo.