KIKOSI cha timu ya Azam FC kimetumia mapumziko ya sikukuu ya Krismasi leo asubuhi kwa kufanya mazoezi ya ukukweni maeneo ya Chadibwa, Kigamboni, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa timu ya Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa ameamua kuwapa programu hiyo wachezaji wake ili kuwaweka fiti kabla ya kuanza kusheherekea sikukuu hiyo.

Programu hiyo imeenda sambamba na maandalizi ya Azam FC kuelekea mechi mbili zijazo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Kagera Sugar keshokutwa na Mtibwa Sugar Jumatano ijayo, zote zikifanyika Uwanja wa Azam Complex.

Katika mazoezi hayo, wachezaji walikimbia mbali mrefu pembezoni mwa bahari hiyo kabla ya kuhamia mazoezi mbalimbali ya kuruka koni kwa staili tofauti na baadaye wakamalizia kwa mazoezi ya kuchezea mpira, wakicheza kwa makundi na kutakiwa kufunga mabao kwenye magoli madogo ya koni.

Aishi Manula arejea dimbani

Jambo zuri la kufurahisha, kikosi cha Azam FC kimeimarika zaidi kuelekea mechi zijazo baada ya kurejea dimbani kwa kipa namba moja Aishi Manula, aliyeumia enka kwenye mchezo uliopita dhidi ya Majimaji, ambao Azam ilishinda mabao 2-1.

Manula alipata majeraha hayo baada ya kukanyagwa mguuni na mchezaji mmoja wa Majimaji kipindi cha kwanza, alipokuwa akiokoa hatari langoni mwake na kupelekea kushindwa kuendelea na nafasi yake ikachukuliwa na kipa Mwadini Ally.

Kabla ya kurejea dimbani leo, Manula alipewa programu maalumu ya siku mbili na Kocha wa Viungo wa Azam FC, Adrian Dobre raia wa Romania, siku ya kwanza alifanya mazoezi ya viungo gym kabla ya jana kufanya mazoezi mengine ya viungo uwanjani na leo akaruhusiwa kuanza kufanya mazoezi na wenzake.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Dobre alisema Manula anaendelea vizuri na yupo katika hali nzuri kucheza huku akisema kuwa suala la kupangwa kwenye mechi zijazo, litakuwa ni jukumu la Kocha Mkuu Stewart Hall.

“Hakuumia sana, alipata mshutuko kwenye enka, tunashukuru Mungu hali yake inaendelea vema, nilimpa programu za siku mbili kufanya mazoezi ya viungo kwanza kuuweka mwili sawa na Ijumaa (leo) ataendelea na mazoezi na wenzake,” alisema Dobre wakati akizungumza na mtandao huu juzi.

Kikosi cha Azam FC jana kiliingia kambini kwenye makao makuu yake ya Azam Complex kuelekea mechi hizo mbili, ambazo ikimaliza itaelekea moja kwa moja visiwani Zanzibar Januari Mosi mchana, kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Azam FC mpaka sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejizolea pointi 29 kati ya 33 kwenye mechi 11 ilizocheza, ina nafasi kubwa ya kurejea kileleni kama ikishinda mechi hizo mbili kwani imezidiwa mchezo mmoja wa kucheza na Yanga iliyo kileleni kwa pointi 30.