TIMU ya Azam FC imefanikiwa kuichapa Majimaji ya Songea mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika jioni ya leo kwenye Uwanja wa Majimaji, mkoani Ruvuma.

Ushindi huo wa Azam FC umeifanya kuisogelea Yanga kileleni yenye pointi 30, baada ya kufikisha jumla ya pointi 29, lakini inazidiwa mchezo mmoja wa kucheza na vinara hao.

Ladha ya mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake, kwa kiasi kikubwa uliathiriwa ubovu wa uwanja huo na mvua kubwa iliyonyesha mkoani Ruvuma na kupelekea baadhi ya maeneo ya Uwanja wa Majimaji kuwa na maji.

Shukrani za pekee ziende kwa washambuliaji wawili wa Azam FC, Didier Kavumbagu na Ame Ally, walioanzishwa kwenye mchezo wa leo sambamba na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na kufunga mabao pekee ya timu hiyo, huku Alex Kondo akifunga kwa upande wa Majimaji.

Azam FC ilianza kuonyesha kuwa imedhamiria ushindi kwenye mchezo huo hasa baada ya kufanya mashambulizi mfululizo katika lango la Majimaji, ilifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 10 kupitia kwa Kavumbagu, aliyeunganisha vema kwa kichwa krosi ya Farid Maliki.

Matajiri hao waliendelea kuliandama lango la wapinzani wao na dakika tisa baadaye ilifanikiwa kupata bao la pili lililofungwa Ame akiunganisha kona iliyochongwa na Farid Maliki.

Mabao hayo yalidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, ambapo kipindi cha pili Azam ilifanya mabadiliko kwa kutoka kipa Aishi Manula, aliyeumia mguu na nafasi yake kuchukuliwa na Mwadini Ally.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kuingia uwanjani na kasi mpya huku zikishambuliana kwa zamu, zote zikitumia mashambulizi ya mipira mirefu na pasi chache.

Majimaji ikajipatia bao la kufutia machozi dakika ya 55 kupitia kwa Kondo aliyefunga kwa kichwa kufuatia kona ya Abubakar Bakar.

Katika kuelekea dakika za mwisho za mchezo huo, Azam FC iligongesha miamba mara tatu kupitia kwa nyota wake, Shomari Kapombe, aliyepiga kichwa kilichogonga mwamba wa juu na kuokolewa na mabeki wa Majimaji, Farid Maliki, naye aipiga shuti lililogonga besela sawa nahodha John Bocco ‘Adebayor’.

Hadi dakika 90 za mwamuzi Anthony Kayombo kutoka Rukwa zinamalizika, Azam FC ilitoka kifua mbele kwa ushindi huo wa tisa msimu huu na ushindi wa nne kwenye mechi zote za ugenini walizocheza, huku akiambulia sare mbili tu dhidi ya Yanga na Simba.

Azam FC itateremka tena dimbani kucheza na Kagera Sugar Desemba 27 kabla ya kukipiga na Mtibwa Sugar Desemba 30 mwaka huu, ukiwa ni mchezo wa kiporo, zote hizo ikicheza Uwanja wa Azam Complex.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa hivi; Aishi Manula/Mwadini Ali dk46, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Serge Wawa, David Mwantika, Farid Maliki, Frank Domayo, Jean Mugiraneza, Ame Ally/Allan Wanga dk85, John Bocco na Didier Kavumbagu.