TIMU ya Azam FC imekuwa gumzo sana hapa Songea tokea ilipowasili mkoani Ruvuma juzi usiku, mashabiki wengi wamekuwa wakiizungumzia mara kwa mara kuekelea mchezo wa jioni ya leo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Majimaji.

Mashabiki wengi mkoani hapa wameanza kupata wasiwasi kuelekea mchezo huo, wakidai kuwa huenda wakakutana na kipigo kikali zaidi ya kile walichopigwa na Toto Africans (5-1) kutokana na ubora wa kikosi cha Azam FC.

Mmoja wa mashabiki hao anayejulikana kwa jina la Idd Hussein, aliuambia mtandao wa azamfc.co.tz kuwa wana kibarua kigumu cha kushinda leo dhidi ya Azam FC.

“Azam FC wako vizuri sana kwanza ukiangalia kikosi chao ni bora kuliko sisi, sisi huku tuna migogoro, tusipoangalia tutafungwa mabao mengi kuliko yale ya Toto Africans,” alisema.

Katika hatua nyingine, Hussein alisema amefurahi sana kuwaona baadhi ya mastaa wa Azam FC kwa mara ya kwanza wakitua mkoani hapa wakiwemo Kipre Tchetche na Pascal Wawa, akidai kuwa ni moja ya wachezaji wenye ubora mkubwa katika ligi hiyo.

Ukiachana na hayo, moja ya jambo kubwa lililozua gumzo zaidi mkoani hapa ni basi la kisasa wanalotumia Azam FC, ambapo wakazi wa hapa wamekuwa wakilishangaa sana na wengine kudiriki kulipa jina la ndege ya ardhini.

Katika mazoezi ya mwisho ya Azam FC jana asubuhi, ilishuhudiwa mamia ya mashabiki mkoani hapa wakijitokeza kwenye Uwanja wa Majimaji kwa kulipa kiingilia na kushuhudia namna timu hiyo inavyojifua.

Wakati Azam FC ikisimamisha jiji la Songea, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Sewart Hall, amesema alipanga kuwapa zawadi ya krismasi mashabiki wa Azam FC kwa kusheherekea sikukuu hiyo wakia kileleni mwa ligi.

“Nilipanga kuwapa zawadi ya krismasi mashabiki wa Azam FC kwa timu kuwa kileleni, lakini hilo halitawezekana kutokana na Yanga kukaa kileleni baada ya kutuzidi idadi ya michezo ya kucheza, lakini nimepanga kuwapa zawadi ya ushindi,” alisema.

Hall alisema watapambana katika mchezo wa leo ili kuhakikisha kuwa wanashinda na kuendeleza vita ya kurejea kileleni huku akidai kuwa anawaheshimu vilivyo wapinzani wao.

“Siwezi kuidharau Majimaji kwa sababu ilifungwa mabao matano na Toto, naiheshimu Majimaji, sitaki kufikiria imejiandaaje, mimi naangalia namna sisi tulivyojiandaa,” alisema.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 26 baada ya kushinda mechi nane na sare mbili, lakini ina nafasi kubwa ya kurejea kileleni kama itashinda mechi ya leo na nyingine mbili zinazokuja dhidi ya Kagera Sugar (Desemba 27) na Mtibwa Sugar (Desemba 30).

Timu hiyo inayomilikiwa na familia ya Mfanyabiashara maarufu Said Salim Bakhresa, mpaka sasa imejizolea rekodi nzuri ya mechi za ugenini na hata nyumbani ikishinda mechi zote tatu ilizocheza, ikizoa pointi sita mkoani Shinyanga kwa kuzifunga Stand United (2-0), Mwadui (1-0) kabla ya kuichapa Ndanda ya Mtwara bao 1-0.