WACHEZAJI wa timu ya Azam FC wameifungia kazi Majimaji ya Songea kwa kuhakikisha wanashinda mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi yao kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea kesho.
Kikosi cha timu ya Azam FC tayari kimeshatua mkoani Ruvuma tokea jana saa 1 usiku na leo asubuhi walifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Majimaji ili kuuzoea kabla ya kucheza na wenyeji wao hao kesho saa 10 jioni.
Hata hivyo uwanja huo umeonekana kuwa kwenye hali mbaya sana katika sehemu ya kuchezea, jambo ambalo limelilazimu benchi la ufundi la Azam FC kubadilisha staili ya uchezaji kwa kutumia sana pasi chache na kupiga mipira mingi ya juu.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo, Nahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’, alisema kuwa wachezaji wenzake wote wapo kwenye morali ya hali ya juu kushinda mchezo huo huku akidai lazima waondoke na pointi tatu katika mchezo huu.
“Tumejipanga vizuri, mazoezi yameenda vizuri na leo tumemaliza mazoezi yetu ya mwisho na wachezaji wote wapo kwenye morali nzuri ya kushinda na naamini kesho tunaenda kutafuta pointi tatu,” alisema.
Bocco alisema sare waliyoipata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba, ndio itawachochea vilivyo kuondoka na ushindi katika mchezo huo ili kuendelea kuifukuza Yanga na kurejea kileleni, ambayo imewazidi michezo miwili mbele ukijumlisha na mechi watakayocheza jioni hii dhidi ya Stand United.
Azam FC mpaka sasa haijafungwa mchezo wowote ikiwa na pointi 26 baada ya kushinda mechi nane na sare mbili ikishika nafasi ya pili, lakini ina nafasi ya kubwa ya kurejea kileleni kama itashinda mechi zote tatu zilizo mbele yake.