KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa vijana wake wamejiandaa vilivyo kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Majimaji ya Songea utakaofanyika Uwanja wa Majimaji Jumapili hii.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo, ikiwa na kiu ya kuendeleza kasi ya kurejea kileleni kwenye msimamo wa ligi kwa kushinda na kufikisha pointi 29 na kuiacha Yanga iliyojikusanyia 27, ambayo imecheza mchezo mmoja mbele dhidi ya Azam FC.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Hall alisisitiza kuwa hawatakuwa na jambo lingine kwenye mchezo huo bali ni kuhakikisha wanashinda.

“Kama unavyoona tumeamua kuja hapa kucheza kwenye uwanja mbovu (DUCE), ili kuzoea mazingira ya uwanja tutakaoenda kuchezea Songea, tumejipanga kushinda mchezo huo na tutapambana kuhakikisha hilo linafanikiwa,” alisema.

Mwingereza huyo alisema kuwa anatarajia kukifanyia mabadiliko kikosi chake kwa kuwachezesha wachezaji watakaoendana na aina ya mchezo wa kupiga mipira ya juu watakaoenda kucheza mkoani Songea.

“Kutakuwa na mabadiliko ndio, natarajia kutumia wachezaji wenye uwezo wa kucheza mipira ya juu na wenye nguvu, kwenye ushambuliaji kutakuwa na mabadiliko, beki pia nitabadilisha na hata eneo la kiungo kutakuwa na mabadiliko,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, Sofapaka, alisema kuwa mechi hiyo haitakuwa rahisi kama wengi wanavyodhania, hasa baada ya Majimaji kufungwa na Toto Africans mabao 5-1 wikiendi iliyopita.

“Hatuangalii matokeo kwa kuwa walifungwa mabao matano, lakini wachezaji wao walikuwa hwajalipwa mishahara kwa muda wa miezi mitatu hivyo hawana moyo, kama kuna mtu atawalipa wiki hii, itakuwa ni timu nyingine tofauti itakayokuwa na moyo.

“Hatudhani kwa kuwa Toto ameshinda mabao matano na sisi tutashinda matano, kwa kuwa hali inaweza kuwa tofauti, kama hujalipwa unakuwa hauna moyo, hivyo tumejipanga kupambana kushinda mchezo huo,” alisema.

Hall alisema anaijua vema Majimaji kutokana na kufanya kazi huko kabla ya kutua Azam FC Mei mwaka huu, akidai kuwa kuna baadhi ya mambo anajua na mengine yamebadilika, lakini hivi sasa ameshapata baadhi ya taarifa zao mpya.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, imepania vilivyo kulitwaa taji la ligi msimu huu walilolitwaa kwa mara ya kwanza 2013/14 bila kufungwa mchezo wowote.