KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya usajili kwa nafasi moja na kuwatoa kwa mkopo wachezaji wengine wanne katika dirisha dogo la usajili lililofungwa nchini saa 6.00 usiku wa kuamkia leo.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz asubuhi ya leo, Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’, alisema mchezaji pekee ambaye wamemsajili ni kipa, Ivo Mapunda.

Usajili wa kipa huyo wa zamani wa Tanzania Prisons, Yanga, St. Georges ya Ethiopia, Gor Mahia ya Kenya na Simba, ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la Azam FC katika kuipa nguvu sehemu ya langoni yenye makipa wengine Aishi Manula na Mwadini Ali.

Benchi la Ufundi chini ya Stewart Hall, limesema kuwa makipa hao watatu watatosha kukabiliana vema na wingi wa michuano iliyo mbele yao, Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Kombe la Mapinduzi, Kombe la FA (Azam Sports Confederation) na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.  

“Lakini kuna vijana wetu wadogo wadogo wanne tmewapeleka kwa mkopo timu nyingine wakapate nafasi ya kucheza na wataanza kucheza mara baada ya taratibu zote za usajili kumalizwa na Kamati ya Usajili na Hadhi za Wachezaji,” alisema.

Wachezaji hao wanaoondoka kwa mkopo ni beki Ismail Gambo ‘Kussi’ aliyeelekea Mwadui ya Shinyanga, kiungo Bryson Raphael amekwenda Ndanda ya Mtwara, kiungo Omary Wayne ametua Coastal Union ya Tanga, huku winga Kelvin Friday akichukuliwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Akitolea ufafanuzi wa suala la Kelvin Friday kwenda Mtibwa, wakati anatakiwa kwenye majaribio katika timu ya St. Georges ya Ethiopia, Father alisema wameamua kufanya hivyo ili kuwahi muda wa usajili wa Tanzania uliofungwa jana na atakwenda huko mambo yakiwa yameshakamilika.

“Kipindi chake cha kwenda kwenye majaribio kipo mbele na dirisha letu la usajili limefungwa jana, tumempeleka huko ili aendelee kucheza wakati akisubiria mambo yake ya kwenda huko kukamilika bahati nzuri kocha aliyemuomba ni Mart Nooij, aliyewahi kuwa Kocha Taifa Stars,” alisema.

Father aliongeza kuwa: “Tayari hivi sasa tumeshatuma passport yake, nyaraka zake kwa ajili ya kumuombea viza, mambo yote hayo yakishakamilika atakwenda mara moja na akifaulu majaribio klabu zote mbili tutakaa chini na kukubaliana. Sisi tunaamini ya kuwa atafaulu na mambo mengine kuendelea.”

Friday, 20, anatakiwa na mabingwa hao wa Ethiopia kwa majaribio ya muda wa wiki moja n tayari uongozi wa Azam FC umepokea kwa mikono miwili suala hilo na umempa baraka zote za kwenda huko mambo yakishakamilika.