TIMU ya Azam FC Academy jana asubuhi iliibana vilivyo klabu ya Polisi Dar es Salaam, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Mchezo huo maalumu wa kirafiki ulifanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, ambapo bao la Azam FC Academy lilifungwa kiufundi na mshambuliaji Shabani Idd.

Licha ya kucheza na timu ya wakubwa, vijana wa Azam walionyesha kiwango kizuri na kutangulia kupata bao kupitia kwa Idd kabla ya Polisi Dar es Salaam kusawazisha kipindi cha pili kuelekea mwishoni mwa mchezo huo.

Huo ni mchezo wa pili Azam FC Academy kucheza ndani ya siku tatu, mwingine walicheza Jumamosi iliyopita kwa kuwafunga vijana wenzao wa Simba mabao 2-1, ikiwa ni mechi ya ufunguzi ya vijana kabla ya ile ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ya wakubwa Azam na Simba iliyoisha kwa sare ya 2-2.

Mechi zote hizo mbili ni sehemu ya programu ya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mwingereza Tom Legg na Msaidizi wake, Idd Cheche, kuwatathimini wachezaji wa timu hiyo pamoja na kuwapa mafunzo.