KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuingia kambini kesho mchana kwenye viunga vya Azam Complex, tayari kabisa kujiandaa kikamilifu kucheza na Majimaji Jumapili hii.

Azam FC itacheza ugenini kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), utakaofanyika katika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema programu ya mazoezi ya kesho itakuwa ni jioni na watafanyia kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE).

“Tumepata uwanja unaoendana na ule wa Majimaji, tunaoenda kuchezea mechi, programu itakuwa tutafanyia Jumatano (kesho) na Alhamisi (keshokutwa),” alisema.

Aliongeza kuwa kikosi hicho kitaanza safari ya kuelekea Songea Ijumaa asubuhi, kwa kupanda ndege na kufikia Mbeya, watakapoanza safari nyingine kwa kutumia basi kubwa la timu hiyo, tayari kabisa kuelekea Songea.

Katika mazoezi ya leo yaliyokuwa yameambatana na mvua za hapa na pale, ilishuhudiwa mabeki watatu, Aggrey Morris, David Mwantika na Racine Diouf wakianza mazoezi ya uwanjani na wenzao baada ya majeraha yao kuimarika.

Mabeki hao jana walipewa programu maalumu ya kufanya mazoezi ya viungo gym, ambapo walikuwa wakisimamiwa kwa ukaribu na Kocha wa Viungo, Adrian Dobre.

Azam FC itaenda kucheza mechi hiyo, ikiwa inajivunia rekodi nzuri ya mechi za ugenini waliyokuwa nayo msimu huu, ikishinda zote tatu walizocheza mpaka sasa kwa kuzifunga Stand United (2-0), Mwadui (1-0) na Ndanda (1-0).

Mpaka sasa Azam FC ipo kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26 baada ya kushinda mechi nane na sare mbili, imefungwa jumla ya mabao saba na kufunga 22, ikifuatiwa na Yanga (24), Mtibwa Sugar (23) na Simba (21).