KOCHA Mkuu wa klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Stewart Hall, amepania kuendelea kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuifunga Majimaji katika mchezo ujao utakaofanyika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea Jumapili hii.

Katika kuhakikisha anatimiza hilo, Hall ameandaa programu maalumu kwa wachezaji wake ya kucheza kwenye uwanja mbovu na kucheza mipira mirefu ya juu.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Hall alisema anafanya hivyo ili kukabiliana na ubovu wa Uwanja wa Majimaji, watakaokwenda kuchezea kwenye mchezo huo.

“Tutatoka nje ya Azam Complex kufanya maandalizi yetu ya mchezo huo, tayari nimeshamwagiza leo mchana, Kocha Dennis (Kitambi) akaangalie uwanja mbovu wa aina ya Majimaji, tutakaotumia kufanyia mazoezi Jumatano na Alhamisi, kabla hatujaelekea Songea,” alisema.

Alisema lazima wafanye maandalizi ya hivyo mapema ili wasipate shida pale watakapocheza na Majimaji kwenye mchezo huo.

Katika mazoezi ya leo wachezaji wote walikuwepo, isipokuwa winga Farid Maliki, ambaye alipewa ruhusu maalumu ya kwenda kushughulikia baadhi ya mambo yake binafsi.

Mabeki wa kati waliokuwa majeruhi Aggrey Morris, David Mwantika na Racine Diouf, wenyewe leo walipewa programu maalumu ya kufanya mazoezi ya viungo gym, wakisimamiwa kwa ukaribu na Kocha wa Viungo wa Azam FC, Adrian Dobre.

Azam FC licha ya kuambulia sare ya mabao 2-2 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Simba, bado imeendelea kutawala kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 26 huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote, ikishinda mara nane na sare mbili.