KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, timu ya Azam FC leo saa 10 jioni itashuka dimbani kuvaana na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo mkubwa utakaokuwa ukifuatiliwa na mashabiki wengi wa soka nchini na nje ya mipaka ya Tanzania, unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na ubora wa timu zote mbili.

Azam FC ndio inaonekana kuwa bora zaidi hasa kutokana na kuwa kileleni mwa ligi mpaka sasa ikiwa imejikusanyia pointi 25 na Simba katika nafasi nne ikiwa nazo 21.

Ubora mwingine wa Azam FC mpaka sasa ni kutofungwa mchezo wowote katika mechi tisa za ligi ilizocheza huku ikifunga jumla ya mabao 20 na kufungwa matano tu, Simba yenyewe imeshapoteza mechi mbili mpaka sasa dhidi ya Yanga na Tanzania Prisons, imefungwa mabao matano na kufunga 15.

Mchezo huo kwa sasa umebatizwa jina la vita vya Waingereza, kutokana na pande zote mbili kuwa na makocha wanaotokea England, Azam FC ikiwa naye Stewart Hall na Simba Dylan Kerr. Hivyo inategemewa kuwa na vita kali ya kimbinu leo.

Kikosi cha Azam FC kipo kamili kwa mchezo huo na kila mchezaji amehamasika kupambana uwanjani kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo, ili kuendelea kukaa kileleni kwenye msimamo wa ligi.

Azam FC itakuwa ikijivunia uwepo wa nyota wake, Kipre Tchetche, ambaye ndiye kinara wa ufungaji mabao wa timu hiyo msimu huu kwenye ligi akiwa ameshafunga mabao saba, Simba yenyewe inaye Mganda Hamis Kiiza aliyefunga nane mpaka sasa.

Benchi la ufundi la Azam FC jana limejinasibu ya kuwa tayari wamemaliza maandalizi ya mchezo huo na kudai kuwa ni lazima waifunge Simba ili kuendelela kukaa kileleni.

Wachezaji pekee wa Azam FC watakaokosekana leo, ni mabeki Racine Diouf na David Mwantika, ambao ni majeruhi huku winga Khamis Mcha ‘Vialli’, akiwa ameelekea visiwani Zanzibar kwa ruhusa maalumu.

Kihistoria timu hizo zimekutana mara 14, tokea Azam FC ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/2009, Azam imeshinda mara nne, Simba mara saba na mechi tatu zimeisha kwa sare.

Katika mechi tisa za ligi ilizocheza mpaka sasa, Azam FC imeshinda mechi nane, tatu kati ya hizo ni za ugenini walizocheza mkoani Shinyanga dhidi ya Stand United (2-0) na Mwadui (1-0) pamoja na ile ya mkoani Mtwara waliyokipiga na Ndanda (1-0), huku ikiambulia sare mchezo mmoja dhidi ya Yanga (1-1).