KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, timu ya Azam FC imekuwa timu pekee ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kupangwa kuanzia raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika mwakani, ikiwa inashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Azam FC itaanza kampeni ya kuwania taji la michuano hiyo kwa kucheza na mshindi wa jumla wa mchezo kati Bidvest Wits ya Afrika Kusini na moja ya klabu kutoka nchini Seychelles ambayo haijajulikana kwa sasa, zote hizo zikianzia raundi ya awali.

Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo iliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana jijini Dakar, Senegal, imeonyesha kuwa Azam FC itaanza kucheza ugenini dhidi ya mojawapo ya timu hizo kati ya Machi 11, 12 na 13 kabla ya kukipiga nyumbani kati ya Machi 18, 19 na 20.

Azam FC inayoongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa na pointi 25, ikifanikiwa kuvuka raundi hiyo itatinga raundi ya pili na kukutana na moja ya timu tatu kati ya Esperance ya Tunisia iliyoanzia raundi ya kwanza, ambayo itatakiwa kupita kwa kucheza na mshindi wa mechi ya raundi ya awali kati ya timu kutoka Chad ambayo haijajulikana na News Stars de Douala ya Cameroon.

Timu hiyo inayomilikiwa na familia ya Mfanyabiashara maarufu nchini na nje ya mipaka ya Tanzania, Said Salim Bakhresa, itacheza mechi za raundi ya pili kwa kuanzia nyumbani kati ya Aprili 8, 9 na 10 na kuhamia ugenini kati ya Aprili 19 na 20.

Baada ya mechi za raundi ya pili, CAF itafanya droo ndogo itakayohusisha timu nane zilizobakia kwenye michuano hiyo, ambazo zitapambanishwa na nane nyingine zilizotolewa katika raundi ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupatikana timu nane za mwisho zitakazotinga hatua ya makundi au robo fainali.

Uongozi wa timu ya Azam FC pamoja na benchi la ufundi, umeweka malengo makubwa kwenye michuano hiyo mwakani ya kufika hatua ya robo fainali, timu hiyo ikiingia hatua hiyo itakuwa ni miongoni mwa timu nane za mwisho zitakazokuwa zikiwania ubingwa huo uliochukuliwa na Etoile du Sahel ya Tunisia mwaka huu.

Ukiiondoa Azam FC, wawakilishi wengine wa Tanzania Bara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga wamepangwa kuanzia raundi ya awali kwa kucheza na Cercle de Joachim ya nchini Mauritius, Yanga itaanzia nyumbani kati Februari 12, 13 na 14 mwakani huku ikimalizia ugenini kati ya Februari 26, 27 na 28.

Ikivuka mtihani huo, itakutana na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland, ikipenya tena hapo itakutana na kigogo kati ya Al Ahly ya Misri au mshindi  jumla wa mchezo kati ya Recreativo de Libolo ya Angola na Racing Micomiseng ya Guinea ya Ikweta.

Kwa upande wa wawakilishi wengine kutoka visiwani Zanzibar katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Mafunzo imepangwa kucheza raundi ya awali kwa kupambana na kigogo AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikipita hapo itakumbana na mshindi wa jumla wa mechi kati ya Mochudi Chiefs ya Botswana na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji.

JKU ya visiwani humo itakayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika, imepangwa kuanza raundi ya awali kwa kucheza na Gaborone ya Botswana, huku ikitakiwa kucheza na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya Khartoum Watani ya Sudan na SC Villa ya Uganda.