KOCHA Msaidizi wa timu ya Azam FC, Dennis Kitambi, amesema kuwa licha ya ugumu wa mchezo wa kesho dhidi ya Simba, ni lazima waifunge timu hiyo ili kuendelea kutetea uongozi wao katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC itaivaa Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku ikiwa kileleni kwa pointi 25 huku wapinzani wao hao wakijikusanyia pointi 21 katika nafasi ya nne kwenye msimamo.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, mara baada ya mazoezi ya leo asubuhi, Kocha Kitambi alisema maandalizi yao yanaendelea vizuri na wamejiandaa na mbinu za kuikabili Simba ikiwemo mfumo wao wanaoutumia.   

Alisema baadhi ya wachezaji watakaoukosa mchezo huo ni mabeki Racine Diouf ambaye ana matatizo ya msuli, David Mwantika aliyeumia kidole gumba wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya African Sports mkoani Tanga pamoja na winga Khamis Mcha ‘Vialli’, aliyepewa ruhusa maalumu ya kwenda Zanzibar kufuatilia mambo yake binafsi.

“Sisi tumejiandaa kwamba tunajua ni mchezo muhimu kwa pande zote mbili, lazima tupate ushindi na wale wachezaji ambao hatukwenda nao Tanga walikuwa kwenye majukumu ya timu za Taifa kwa hiyo wamerudi na wiki hii nzima tumepata muda wa kufanya nao kazi kwa hiyo hilo ni jambo jema.

“Kikubwa kabisa ambacho sisi tunaamini kabisa mchezo huu ni timu mbili ambazo katika ligi kwa ujumla ukiangalia ndizo zinazotumia mifumo miwili tofauti ukilinganisha na timu nyingine zote, kwa hiyo hasa hasa maandalizi yetu yamelenga katika suala la zima la mbinu za kukabiliana na mfumo wa Simba.

“Na pia vilevile jinsi ambavyo sisi tunavyoweza kujiboresha kutokana na kwamba ndio tumeweza kufika katika hatua ya sisi tunaongoza ligi, lakini tunatambua ya kuwa tayari makocha wengine watakuwa wshasoma uzuri wetu na mapungufu yetu kwa hiyo sisi tumeangalia pia namna gani ambavyo tunaweza kuboresha uchezaji wetu,” alisema.

Kocha huyo aliyepata mafunzo ya ukocha nchini England alisema kuwa wanatambua ya kuwa Simba itaingia kwenye mchezo huo ikitaka kushinda na kutokana na namna wanavyojiona na muda mrefu hawajacheza michuano ya kimataifa, hivyo msimu huu wanataka kujaribu kuipata nafasi hiyo.

Wachezaji wote wa Azam FC wana ari kubwa ya kushinda mchezo huo na hata katika mazoezi yote waliyofanya ya kujiandaa na mchezo huo, kila mchezaji amekuwa akionyesha kiwango cha hali ya juu ili kuwashawishi makocha wampange katika mechi hiyo.