KIPA wa timu ya Azam FC, Khalid Mahadhi Haji, leo ameuaga ukapera baada ya kufunga ndoa na Bi. Khairat Mohamed Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kufunga ndoa hiyo, Mahadhi aliwapongeza wachezaji wenzake na wafanyakazi wa Azam FC waliofika kwa wingi kwenye harusi yake hiyo ili kumpa sapoti.

“Nimefurahi sana na naamini kwamba nyie ndio ambao ni nguzo mtakaonifanya niweze kuhudumu katika ndoa yangu, kuwepo kwenu ndio kunifanya mimi kuweza kuishi vizuri katika maisha yangu ya familia.

“Pia kuweza kuitunza familia yangu kwa sababu thamani yenu ya kufika hapa nitaithamini sana na nitamuomba Mungu anijalie niweze kuwapenda zaidi na kufahamiana zaidi,” alisema.

Mahadhi ni mtoto wa tisa wa kuzaliwa kwenye familia ya Mzee Mahadhi Haji, ambapo anafunga ndoa hiyo akiwa ndio kwanza amefikisha umri wa miaka 29.