TIMU ya Azam FC imerejea salama jijini Dar es Salaam leo mchana ikitokea ziarani mkoani Tanga, ilipokwenda kusaka makali ya kujiandaa na mchezo muhimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba Desemba 12, mwaka huu.

Azam FC katika kumalizia maandalizi yake ya mwisho kuelekea mchezo huo, kesho Jumatatu saa 8 mchana inatarajia kuingia kambini tayari kabisa kuwavutia kasi Simba.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Jaffar Idd, ameuambia mtandao wa azamfc.co.tz, kuwa wachezaji wote walikwenda ziarani mkoani Tanga na wale waliokuwa kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, wanatarajia kujumuika pamoja kesho kwenye mazoezi ya kwanza.

“Tutaingia kambini kesho saa 8 mchana, ndio itakuwa moja kwa moja hadi tunacheza na Simba, kikubwa ni maandalizi, kama unavyojua maandalizi yetu tumeanzia Tanga, hivyo kuanzia kesho tutafanya maandalizi ya mwisho mwisho,” alisema.

Idd alisema malengo yao kuelekea mchezo wa Simba ni kupambana na kuibuka na pointi tatu ili kuendelea kukaa kileleni mwa ligi.

Baadhi ya wachezaji waliokuwa kwenye michuano ya Chalenji nchini Ethiopia, watakaoripoti kwenye mazoezi ya kesho jioni baada ya kuingia kambini ni nahodha John Bocco ‘Adebayor’, nahodha msaidizi Himid Mao ‘Ninja’, Shomari Kapombe, Ame Ally ‘Zungu’, Mudathir Yahya, Aishi Manula, ambao wote waliikosa kambi ya mkoani Tanga.

Wakati huo huo, mshambuliaji raia wa Burundi Didier Kavumbagu, ambaye naye alikuwa kwenye michuano ya Chalenji, ametua nchini leo tayari kwa kuanza kujifua kesho kwa ajili ya mchezo huo, huku Allan Wanga kutoka Kenya akitarajiwa kuwasili nchini kesho asubuhi baada ya kukosa tiketi ya ndege ya kutua leo.

Ikiwa mkoani Tanga kwa siku tano, Azam FC ilifanikiwa kucheza mechi mbili za mazoezi za kirafiki dhidi ya Mgambo JKT na African Sports, ambazo zote ziliisha kwa sare ya bao 1-1.

Malengo makuu ya benchi la ufundi kucheza mechi hizo mbili za kirafiki, ilikuwa ni kuwamulika kiufundi wachezaji waliokuwa hawajapata nafasi ya kucheza muda mrefu baada ya ligi kusimama, ikiwa pia kupima ufiti wao na kuwapa baadhi ya mbinu.