KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imemaliza ziara ya siku tano mkoani Tanga kwa kutoka sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya African Sports kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani jioni ya leo.

Awali juzi ilianza kwa kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Mgambo JKT na kutoka sare ya 1-1, bao la Azam FC likifungwa na Kipre Tchetche dakika 13 huku la Mgambo likipigwa na Fully Maganga dakika 87.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alifanya mabadiliko mawili kikosini kwenye mchezo wa leo, akimwanzisha langoni kipa mpya mkongwe Ivo Mapunda badala ya Mwadini Ally na kumpumzisha beki Gardiel Michael na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Maliki.

Kipa Ivo Mapunda kucheza mchezo huo kumemfanya awe amedaka mchezo wake kwanza ndani ya timu hiyo tokea asajiliwe kwenye usajili huu wa dirisha dogo.

Azam FC iliuanza kwa kasi mchezo huo ikitaka kupata bao la mapema, lakini umakini wa safu ya ushambuliaji na umakini wa mabeki wa African Sports uliwanyima mabao.

Dakika ya 36, almanusura mshambuliaji Kipre Tchetche, aipatie bao la uongozi Azam FC baada ya mpira safi wa adhabu ndogo alioupiga kwenye umbali wa takribani mita 30, kupanguliwa vema na kipa wa African Sports.

Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza za mwamuzi Ibrahim Kidiwa kutoka Tanga, zinamalizika, timu zote zilienda vyumbani mapumziko milango ikiwa ni migumu.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam FC kufanya mabadiliko kwa kuingia mabeki Said Morad ‘Mweda’ na David Mwantika wakichukua nafasi za Racine Diouf na Abdallah Kheri ‘Sebo’.

Azam FC iliyokianza kwa kasi kipindi hicho, ilifanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 46 kupitia kwa beki mkongwe wa timu hiyo, Erasto Nyoni, aliyepiga shuti baada ya kuinasa pasi ya kiungo mahiri Frank Domayo ‘Chumvi’.

African Sports walicharuka baada ya kufungwa bao hilo na hatimaye wakasawazisha dakika ya 56 kwa njia ya mkwaju wa penalti uliopigwa na Rashid Ismaily.

Baada ya African Sports kupata bao hilo, mpira huo ulionekana kuwa mkali sana kwa timu zote kushambuliana kwa zamu kwa kasi kubwa, huku Azam FC ikionekana kulifikia sana lango la wapinzani wao, ambao walikuwa wakitumia mashambulizi ya kushtukiza kupitia pembeni. 

Hadi dakika 90 zinamalizika, timu hizo zilitoshana nguvu.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, mara baada ya mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, alisema lengo lao kubwa liliwafanya waweke kambi mkoani humo limetimia kwani baadhi ya wachezaji waliokuwa hawajapata nafasi ya kucheza muda mrefu wameonyesha viwango vizuri.

“Lengo letu limetimia kwani baadhi ya wachezaji tuliokuja nao walikuwa wanahitaji kucheza, kwa hiyo tumewapa nafasi ya kucheza na tumeona kabisa kuna mabadiliko, na pia kuna jambo la kiufundi tulikuwa tunajaribu, tumefanya jaribio hilo kwenye mchezo uliopita kwa hiyo tumepata majibu nini kinachoweza kufanya kazi na kipi hakiwezi kufanya kazi,” alisema.

Kocha huyo kijana aliyepata mafunzo ya ukocha nchini Uingereza, aliongeza kuwa: “Kwa ujumla sisi tumeridhika na ziara yetu ya huku kuja Tanga.”

Moja ya malengo makubwa ya Azam FC kwenye kambi ya jijini Tanga, ilikuwa ni kuwapa nafasi wachezaji ambao walikuwa mapumzikoni kujiweka fiti kwa kucheza mechi mbili za kirafiki na mazoezi makali ya ufiti.

Azam FC kesho Jumapili itaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam mapema saa 12 asubuhi, ambapo itaongezewa nguvu kwa urejeo wa baadhi ya nyota wake waliokuwa kwenye michuano ya Kombe la Chalenji nchini Ethiopia.

Kikosi Azam: Ivo Mapunda 3, Erasto Nyoni 6, Farid Mussa 17, Abdallah Kheri 25, Pascal Wawa 5, Racine Diouf 21, Michael Bolou 29, Frank Domayo 18, Ramadhan Singano 14, Kipre Tchetche 10, Shaaban Idd 43.

Walioingia: Kheri/Said Morad 15 (dk 45), Diouf/David Mwantika 12 (dk 45), Idd/Khamis Mcha ‘Vialli’ 22 (dk 45), Farid/Gardiel Michael 2 (dk 58), Nyoni/Wazir Salum 26 (dk 77).

Hawakucheza: Mwadini Ali 1, Masoud Abdallah 34.