KAMBI ya Azam FC imeendelea tena kwa siku ya tatu jijini hapa Tanga kwa wachezaji kufanya mazoezi ya kwanza baada ya kucheza mchezo wa kirafiki jana dhidi ya Mgambo JKT.

Azam FC imeweka kambi ya siku tano mkoani hapa ikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba, utakaofanyika Desemba 12, mwaka huu.

Mazoezi ya leo yameonekana kunoga sana, licha ya wachezaji kujifua juani kuanzia saa 4.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa, ambayo yalichukua takribani saa moja na robo.

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Stewart Hall na Msaidizi wake, Dennis Kitambi, walitoa mazoezi kadhaa kwa wachezaji ya kuwajengea ufiti pamoja kasi yakiwemo mazoezi mbalimbali ya namna ya kucheza na mipira.

Kocha wa Makipa, Idd Abubakar, naye alikuwa bize kuwanoa vikali makipa wawili walioko mkoani hapa kipa mpya Ivo Mapunda na Mwadini Ali, walipewa baadhi ya mazoezi ya kurukia mipira ya juu, chini na pembeni.

Baada ya mazoezi hayo kiungo fundi, Frank Domayo ‘Chumvi’, aliuambia mtandao wa azamfc.co.tz kuwa kambi waliyoweka jijini Tanga ni nzuri huku akifurahishwa na namna makocha wanavyowapa mafunzo mbalimbali.

“Mazingira ya kambi sisi tunayaona mazuri kabisa, tumefurahia sisi kuja kuweka kambi hapa na hata mafunzo tunayopewa ni mazuri,” alisema beki wa mkongwe wa kushoto wa Azam FC, Erasto Nyoni.

Naye beki wa kati kisiki Said Morad ‘Mweda’ alisema: “Kambi tunamshukuru Mungu mpaka sasa ipo salama hatuna majeruhi na mechi inayokuja dhidi ya Simba ni mgumu na sio nyepesi, inatakiwa kujitahidi na tukipata nafasi tuitumie.”

Kwa upande wake winga machachari, Khamis Mcha ‘Vialli’, alisema kambi yao ipo vizuri pamoja na mafunzo wanayopewa huku akidai kuwa wanauhakika wa kuifunga Simba na kumwomba Mungu awajaalie kwa hilo.

Baada ya mazoezi ya leo Azam FC kesho saa 10.30 jioni itahitimisha mechi yake ya pili ya kirafiki kwa kucheza na African Sports ya jijini hapa na Jumapili asubuhi itaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, tayari kabisa kwa maandalizi ya mwisho mwisho kabla ya kuivaa Simba.