TIMU ya Azam FC imetoka sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wa kirafiki mkoani Tanga dhidi ya wenyeji wao Mgambo JKT, uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani jioni ya leo.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 13, lililofungwa kiufundi na straika hatari Kipre Tchetche, aliyeitendea haki pasi safi ya mbali ya pacha wake, Michael Bolou.

Azam FC iliendelea kutawala mchezo huo na kutengeneza nafasi nyingine, ambazo zilishindwa kutumiwa vema na kupelekea kwenda mapumziko kwa uongozi wa bao hilo moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Mkuu wa Azam FC kufanya mabadiliko kwa kuwapumzisha mabeki Racine Diouf, Pascal Wawa na kuwaingiza David Mwantika na Said Morad ‘Mweda’.

Hall pia alimtoa kinda Shaaban Idd na kumuingiza Khamis Mcha ‘Vialli’, pia aliingia Farid Mussa kuchukua nafasi ya Ramadhan Singano ‘Messi’.

Kipindi cha pili Mgambo ilionekana kubadilika sana na kucheza vema kuliko kipindi cha kwanza, ambacho Azam FC ilikitawala kwa asilimia kubwa.

Katika mchezo huo dakika ya 78 ilishuhudiwa beki wa kushoto wa Azam FC, Wazir Salum, akichukua nafasi ya Erasto Nyoni na kucheza mechi yake ya kwanza baada ya kipindi cha mwaka mmoja alichokuwa akitumia kuuguza majeraha.

Azam FC ilifanya mabadiliko mengine kwa kuingia kinda Prosper Joseph, aliyechukua nafasi ya nahodha wa mchezo wa leo, kiungo Michael Bolou, ambaye alimkabidhi kitambaa cha unahodha beki Said Morad.

Mgambo JKT ilifanikiwa kujipatia bao la kusawazisha dakika ya 87, lililofungwa na Fully Maganga, aliyepokea pasi ya juu na kuutuliza mpira kisha kufunga bao hilo.

Baada ya kumalizika mchezo huo, Kocha Mkuu Hall, alisema Azam FC ilicheza vema kipindi cha kwanza kwa kuumiliki mchezo huo kama Mgambo ilivyofanya kipindi cha pili.

“Matokeo ya sare ya 1-1 yamestahili kwa pande zote mbili, kipindi cha pili wachezaji wangu walichoka na ufiti wao ulikuwa katika kiwango cha chini, hii ilitokana na baadhi ya wachezaji waliocheza kucheza kwa mara ya kwanza baada ya kutoka kwenye majeruhi,” alisema.

Hall alisema alitumia mchezo huo kuwaongezea ufiti wachezaji wake na pia kujaribu mfumo wake mwingine wa 3-4-3 huku akidai kuwa atarejea kwenye mfumo wake wa awali wa 3-5-2 katika mchezo ujao wa kirafiki dhidi ya African Sports utakaofanyika Jumamosi ijayo.

Azam FC imeweka kambi mkoani Tanga kwa ajili ya kujiandaa na vilivyo na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba.

Itaingia kwenye mchezo huo ikiwa kileleni kwenye msimamo ikiwa na pointi 25 baada ya kushinda mechi nane na sare moja huku Simba ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 21.

Kikosi:

Mwadini Ali, Abdallah Kheri, Pascal Wawa (Said Morad dk45), Racine Diouf (David Mwantika dk45), Erasto Nyoni (Wazir Salum dk 78), Gardiel Michael, Frank Domayo, Michael Bolou (Prosper Joseph dk82), Ramadhan Singano (Farid Mussa dk45), Shaaban Idd (Khamis Mcha dk45), Kipre Tchetche