WINGA wa timu ya Azam FC, Kelvin Friday, amewavutia mabingwa wa Ligi Kuu Ethiopia, St. Georges baada ya klabu hiyo kutuma barua ya kumtaka kinda huyo akafanye majaribio.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema tayari wamepokea barua rasmi ya mwaliko huo kutoka kwa mabingwa hao na sasa inashughulikiwa.
“St. Georges inamtaka Kelvin Friday kwa majaribio ya wiki moja, imeshatutumia barua rasmi leo na sasa tunaifanyia kazi kwani ndio tumeipokea asubuhi hii, hivyo kwa baadaye tutajua anatakiwa kwenda huko lini baada ya kuwasiliana nao,” alisema.
Friday ni mmoja ya wachezaji waliokulia kwenye Azam FC Academy na kupandishwa timu kubwa, moja ya sifa yake kubwa ni uwezo wa kupiga mashuti ya mbali.
St Georges hivi sasa inafundishwa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mholanzi Mart Nooij, ambaye amewahi kumuita mara kwa mara Friday kwenye kikosi cha Stars akianzia na Taifa Stars Maboresho.