KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC imewasili salama mkoani Tanga leo saa 12 jioni tayari kabisa kwa kambi ya siku tano ya kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Desemba 12, mwaka huu.

Msafara wa Azam FC uliowasili mkoani hapa umetumia takribani masaa nane njiani hadi inawasili, ilianza safari hiyo saa 4.30 asubuhi kwenye Makao Makuu, Azam Complex.

Baada ya kuwasili, Azam FC inatarajia  kuanza kambi hiyo kwa kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya Mgambo JKT kesho, mechi itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa, kuanzia majira ya saa 10.30 jioni kabla ya Jumamosi ijayo kumaliza ziara hiyo kwa kukipiga na African Sports.

Wachezaji waliowasili mkoani hapa ni makipa Ivo Mapunda na Mwadini Ally, mabeki Pascal Wawa, David Mwantika, Said Morad ‘Mweda’, Erasto Nyoni, Racine Diouf, Waziri Salum, Abdallah Kheri ‘Sebo’, Gardiel Michael.
Wengine ni viungo Frank Domayo ‘Chumvi’, Michael Bolou, Ramadhan Singano ‘Messi’, mawinga Khamis Mcha ‘Vialli’ na Farid Maliki, mshambuliaji Kipre Tchetche pamoja na wachezaji watatu wa Azam Academy, Shabani Idd, Masoud Cabaye na Prosper Mushi.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz leo asubuhi kabla ya safari hiyo, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema wachezaji wengine waliobakia Dar es Salaam ni wale baadhi waliokuwa kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, ambao wikiendi hii wataanza mazoezi chini ya Kocha Msaidizi, Mario Marinica.
“Bocco (John), Himid Mao, walicheza mechi nne za CECAFA, Kapombe (Shomari) naye sitamtumia, wengine Allan Wanga, Ame Ally, Mudathir Yahya nao watabakia hapa (Dar es Salaam), watafanya mazoezi na Mario (Marinica) Jumamosi na Jumapili kabla ya Jumatatu kuungana na sisi baada ya kurejea.
“Vilevile Aggrey Morris naye atabakia bado anasumbuliwa na maumivu ya mguu, hivyo atakuwa akipewa matibabu na mazoezi ya viungo,” alisema.