MABINGWA wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, timu ya Azam FC kesho Jumatano inatarajia kwenda ziarani Tanga kwa ajili ya kujiandaa vema na mechi zilizo mbele yake.

Ofisa Mtendaji wa Azam FC, ameuambia mtandao wa azamfc.co.tz leo kuwa timu ikiwa huko itacheza mechi za kirafiki za kujipima nguvu dhidi ya Mgambo JKT itakayofanyika Desemba 3 na nyingine watacheza na African Sports Desemba 5, mwaka huu.

“Mechi zote hizo zitafanyika Uwanja wa CCM Mkwakwani na mara baada ya kumaliza mechi zote itarejea jijini Dar es salaam Desemba 6 mwaka huu,” alisema.

Azam FC imeonyesha ubora mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu ikiwa inaongoza kwa pointi 25, ikishinda mechi nane kati ya tisa ilizocheza na kuambulia sare moja.

Desemba 12, mwaka huu itakabiliwa na mchezo muhimu wa kuendeleza rekodi yake hiyo kwa kucheza na Simba, iliyo nafasi ya nne kwa pointi 21.