NYOTA wa timu ya Azam FC, beki kisiki Aggrey Morris na winga Farid Maliki, wameanza rasmi mazoezi ya uwanjani baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakiwakabili.

Wachezaji hao waliumia wakati wakiwa kwenye kambi za timu za Taifa, Morris alipata majeraha akiwa na Zanzibar Heroes na Maliki Taifa Stars katika mchezo dhidi ya Algeria.

Jicho la azamfc.co.tz limewashuhudia wawili hao wakifanya mazoezi ya nguvu jana asubuhi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, ambapo walionekana kurejea vizuri tayari kabisa kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) dhidi ya Simba, utakaofanyika Desemba 12, mwaka huu.

Mbali na urejeo wa wachezaji hao, mazoezi ya jana yameonekana kunoga sana kutokana na wachezaji wa timu kubwa na wale wa academy kujituma vilivyo kwenye kila zoezi walilopewa na benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall, Kocha Msaidizi, Dennis Kitambi pamoja na Kocha Mkuu wa Azam Academy, Tom Legg.

Cha kuvutia zaidi walikuwa wakifanya mazoezi huku mvua ikiwa inanyesha kwenye baadhi ya muda.

Hii ni siku ya sita tokea Azam FC ianze mazoezi yake, ambapo bado inaendelea kuwakosa nyota 12 wa timu kubwa, ambao wapo nchini Ethiopia wakishiriki michuano ya Kombe la Chalenji.

Muda wowote kuanzia kesho, wachezaji 10 watarejea kikosini baada ya timu zao kutolewa kwenye michuano hiyo.

Wachezaji hao ni kipa Aishi Manula, beki Shomari Kapombe, viungo Himid Mao, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, nahodha John Bocco ‘Adebayor’ (Kilimanjaro Stars), kipa Mwadini Ally, kiungo Mudathir Yahya ‘Muda’, winga Khamis Mcha ‘Vialli’, Ame Ally ‘Zungu’ (Zanzibar Heroes) na Didier Kavumbagu (Burundi).

Itaendelea kuwakosa nyota wawili Allan Wanga (Kenya) na Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ (Rwanda), ambao timu zao leo zitakutana kwenye robo fainali ya Kombe la Kagame.

Vilevile nyota wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Pascal Wawa, yeye anatarajia kutua nchini leo na kuingia moja kwa moja kambini.

Kocha Stewart Hall, bado amesisitiza kuwa amelazimika kusitisha baadhi ya program zake za kiufundi kutokana na kuwakosa wachezaji wake wengi wa timu kubwa na anawasubiria hao ili kuanza kutoa mbinu za kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba.