KOCHA Mkuu wa timu ya Azam FC, Stewart Hall, amesema kuwa kwa sasa anawapa zaidi wachezaji wake mazoezi ya kuwaweka fiti kimwili kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Simba utakaopigwa Desemba 12, mwaka huu.

Hall ameiambia azamfc.co.tz leo asubuhi kwenye mazoezi ya ufukweni katika fukwe za Coco Beach, kuwa ataanza rasmi kuwapa mafunzo ya kiufundi pale nyota wake 12 walioko timu za Taifa wakishiriki Kombe la Chalenji, watakaporejea kikosini.

“Wachezaji walikuwa kwenye mapumziko ya wiki tatu, wamerejea wiki hii mazoezini, kwa sasa tunafanya zaidi mazoezi ya kuwaweka fiti, hatuwezi kufanya mazoezi ya kiufundi kwa kuwa tuna wachezaji tisa tu wa timu kubwa, wachezaji 12 wengine wapo kwenye michuano ya CECAFA, wachezaji wawili majeruhi (Aggrey Morris na Farid Maliki).

“Hivyo ni vigumu kwa sasa kufanya mazoezi ya kiufundi kama huna wachezaji wengi wa timu kubwa,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Zanzibar Heroes na Sofapaka ya Kenya, aliongeza kuwa: “Kwa sasa hatujaanza kujiandaa na mchezo huo, Simba ina faida kubwa kuliko sisi kuelekea mechi hiyo, kwa kuwa wao wana wachezaji saba wapo timu za Taifa, sisi wetu ni wengi zaidi tukiwa nao 12, mazoezi rasmi ya kiufundi tutaanza baada ya kurejea wachezaji hao.”

“Huwezi kujua nani aterejea akiwa ameumia, Himid Mao anaweza kurejea akiwa ameumia, vivyo hivyo kwa Bocco (John) na Aishi Manula, hilo linaweza kuharibu kile ulichokuwa ukifikiria kuelekea mchezo huo.

“Hivyo tunasubiria kuona namna wachezaji wetu watakavyorejea kutoka CECAFA na kuangalia nani yupo fiti na baada ya hapo ndio uamue namna gani unakwenda kucheza kiufundi dhidi ya Simba,” alisema. 

Mpaka sasa Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ndio vinara wa ligi kwa pointi 25, wakiwa wamecheza mechi tisa, wakishinda nane na kutoa sare mchezo mmoja dhidi ya wanaoshika nafasi ya pili Yanga waliojikusanyia 23.