KIPA namna moja wa timu ya Azam FC, Aishi Manula, amefichua siri ya kudaka penalti nyingi, akidai kuwa kuna mambo makuu matatu huyazingatia.

Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz hivi karibuni, Manula alisema cha kwanza ambacho huwa anafikiria ni kudaka penalti hiyo na si kitu kingine.

“Na ninapofikiria kudaka penalti kuna vitu vingi huwa nawaza, kwamba nitadaka kwa staili gani kutokana na mtu anayeenda kupiga, lazima pia kitu cha pili lazima nijue anayepiga anatumia mguu gani kama ni wa kushoto au kulia.

“Nitakapojua anatumia mguu wa kushoto au kulia, kinachofuata ni kuangalia amekaa mkao gani wa kupiga ule mpira, kwa hiyo kuna mikao mingi tofauti akikaa ninaweza nikajua pale anapiga upande gani,” alisema.

Akizungumzia hisia za baadhi ya watu wanaodai ya kuwa anabahatisha, alidai kuwa: “Kitu kikubwa kwenye penalti ni hicho kukisia, hivyo ukishamwangalia anayepiga kakaaje, unaweza ukajua asilimia 90 huyu mtu anapiga huku.”

Utofauti wa penalti

“Kuna tofauti kubwa kati ya penalti ile ya moja kwa moja na ile ya baada ya dakika 90, penalti za baada ya dakika 90 kuisha, mpigaji huwa amejiandaa kwa kujua saivi ni hatua ya kupiga panalti, hivyo kwa golikipa inakuwa ni changamoto kubwa, lakini ile ya ndani ya dakika 90 huwa inatokea tu na mpigaji anakuwa hajajiandaa,” alisema       

Mbwembwe zinahusika

Manula alizungumzia mbwembwe zake za kurukaruka langoni na kuushika mpira kabla ya penalti kupigwa na kudai kuwa mambo hayo husaidia sana kumwogopesha mpigaji.

“Unajua katika pigo la penalti au katika kitu chochote, vile wewe unavyojiweka wakati mwingine matokeo yanakuja vilevile ulivyokuwa umejiweka, unapokuwa mnyonge mnyonge katika mpira, unakuwa umempa nafasi mpinzani wako kujiamini na kukushinda, lakini ukiwa unajiamini lazima ajiulize kwa nini huyu anajiamini, hapo hapo ndipo unapomshinda,” alisema.

Awaonyesha Yanga, Mwadui

Msimu huu wa ligi mpaka sasa, Manula ameshadaka penalti mbili, zote amedaka na kuipa Azam FC pointi muhimu, alidaka ya kwanza iliyopigwa na Rashid Mandawa wa Mwadui waliposhinda bao 1-0, kabla ya kumdakia kiungo Thabani Kamusoko wa Yanga kwenye sare ya bao 1-1.