TIMU ya Azam FC kesho itaanza rasmi mazoezi kujiandaa na mwendelezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine.

Benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall, liliwapa mapumziko ya wiki tatu wachezaji mara baada ya kumalizika kwa mechi ya raundi ya tisa ya ligi dhidi ya Toto Africans, iliyoisha kwa Azam FC kushinda mabao 5-0.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Idd, ameiambia azamfc.co.tz leo kuwa, mazoezi hayo yatahusisha wachezaji takribani 10 wa timu kubwa watakaochanganyika na timu ya vijana ya timu hiyo.

Azam FC kwenye mazoezi hayo, itawakosa wachezaji takribani 12 waliokuwa timu za Taifa za Tanzania Bara, Zanzibar, Rwanda, Burundi na Kenya, wakishiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Ethiopia hadi Desemba 6, mwaka huu.

“Timu itaanza na mazoezi mepesi kesho asubuhi, ikiwasubiria nyota waliokuwa timu za Taifa, kutokana na upungufu wa wachezaji wengi wa timu kubwa, watachanganyika na wachezaji wa timu ya vijana,” alisema.