JUMLA ya wachezaji 10 wa Azam FC wanaunda vikosi vya wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, timu ya Taifa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na Zanzibar Heroes.

Michuano hiyo mwaka huu itafanyika nchini Ethiopia kuanzia Jumamosi Novemba 21 hadi Desemba 6 mwaka huu na kushirikisha jumla ya mataifa 11 ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na mwalikwa Malawi ‘The Flames’.

Kocha wa Kili Stars, Abdallah Kibadeni ‘King’, ameita wachezaji 21 watakaoshiriki michuano hiyo huku wachezaji watano wakitoka Azam FC, ambao ni kipa Aishi Manula, beki wa kulia Shomari Kapombe, viungo Himid Mao ‘Ninja’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’ (nahodha).

Wengine wanaunda kikosi hicho ni makipa Ally Mustafa (Yanga) na Said Mohamed (Mtibwa Sugar). mabeki Hassan Kessy, Mohammed  Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka (Simba), Salim Mbonde (Mtibwa), Juma Abdul na Kelvin Yondani (Yanga).

Viungo Jonas Mkude, Said Ndemla (Simba), Salum Telela, Deus Kaseke (Yanga), washambuliaji ni Elias Maguri (Stand United), Ibrahim Ajibu (Simba), Malimi Busungu na Saimon Msuva (Yanga).

Kwa upande wa Zanzibar Heroes, Kocha Msaidizi Malale Hamsini, naye ameteua nyota 21 wakiwemo watano pia kutoka Azam FC ambao ni kipa Mwadini Ali, beki wa kati Aggrey Morris, kiungo Mudathir Yahya, winga Khamis Mcha ‘Vialli’ na mshambuliaji Ame Ali ‘Zungu’.    

Walioitwa wengine ni kipa Mohammed Abrahman (JKU), mabeki  Nassor Masoud ‘Chollo’ (Stand United), Ismail Khamis (JKU), Adeyum Saleh (Coastal Union), Mwinyi Haji (Yanga), Issa Haidar (JKU), Said Mussa ‘Udindi’ (Mafunzo), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga).

Viungo ni Said Juma Makapu (Yanga), Awadh Juma (Simba), Omar Juma (Chipukizi), Suleiman Kassim ‘Selembe’ (Stand United), Mohammed Abrahman (Mafunzo) huku washambuliaji wakiwa ni Matheo Simon (Yanga) na Ibrahim Hilika (Zimamoto).

Jumla ya makundi matatu yamepangwa kuelekea michuano hiyo, Kili Stars ipo Kundi A sambamba na wenyeji Ethiopia, Somalia na Rwanda, Zanzibar Heroes ipo Kundi B pamoja na bingwa mtetezi Kenya, Burundi na Uganda huku Kundi C likiwa limebeba timu za Sudan, Sudan Kusini, Djibouti.

Uongozi wa Azam FC unapenda kuzitakia maandalizi mema na mafanikio timu za Tanzania kuelekea michuano hiyo ili waweze kurudi na ubingwa nchini.