TIMU ya Azam FC imeendelea kuongoza kwa ubora miongoni mwa timu za Tanzania, kwa mujibu viwango vya ubora vilivyotolewa na mtandao wa footballdatabase.com Novemba 15, mwaka huu.

Mtandao huo umekuwa ukizichambua klabu mbalimbali duniani na kuzipa viwango kila mwezi kutokana na matokeo wanayopata kwenye mechi zao.

Azam FC inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), inakamata nafasi ya 334 Afrika ikiwa imepanda nafasi 88 baada ya kujizolea jumla ya pointi 1249.

Klabu nyingine ya Tanzania iliyoorodheshwa kwenye mtandao huo ni Simba, ambayo inafuatia katika nafasi ya 338 ikipanda nafasi 86 ikiwa imejisanyia pointi 1247.

Ni klabu hizo tu za Tanzania zilizochaguliwa na mtandao huo, ambao uhusisha timu 405 kutoka Afrika.

Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu, TP Mazembe kutoka DRC yenye urafiki wa karibu na Azam FC, ndio kinara kwa upande wa Afrika ikiwa imejizolea pointi 1653 ikifuatiwa na wapinzani wao Vita Club, El Merreikh (Sudan) na Esperance de Tunis na Kaizer Chiefs.