WANAFUNZI wa kituo cha elimu cha ‘Master the Great Education Center’ cha Charambe Foma na Mbagala Kizuiani, leo wametembelea viunga vya Azam Complex na kuadhimisha siku yao ya michezo ‘Sports Day’.

Hii ni mara ya pili kwa kituo hicho kufanya ziara ndani ya viunga hivyo, safari hii wamehudhuria wanafunzi takribani 600, wasichana kwa wavulana wanaosomea mafunzo ya awali kabla ya kuingia kidato cha kwanza mwakani ‘Pre Form One’.

Siku yao ilifana sana baada ya kufaidika vilivyo na ubora wa Uwanja wa Azam Complex, wakishiriki michezo ya soka na riadha huku wanawake wakicheza mchezo wa rede mstari.

Wanafunzi hao pia walipata fursa ya kuonana ana kwa ana na mchezaji nyota wa Azam FC, beki kisiki wa kati Said Morad na kuwafundisha mambo mbalimbali ya soka pamoja na kujibu maswali kutoka kwao.

Mmiliki wa kituo hicho, Amini Abdul Rajab, aliuambia mtandao huu kuwa, wamefurahishwa sana na kuitembelea Azam FC na kudai kuwa wanafunzi wamekuwa wakifurahia sana safari hiyo, jambo ambalo linawalazimu kila mara kufanya shughuli zao za michezo kwenye uwanja huo.
 

Naye mmoja wa wachezaji chipukizi wa kituo hicho, ambaye ni mfungaji bora wa Ligi ya Kizuiani akifunga mabao saba, Mohamed Kingo (13), alisema kwa ufupi kuwa: “Nina furaha sana kuwa hapa Azam FC ni klabu kubwa sana iliyofanya uwekezaji kuliko timu nyingine ya hapa, malengo yangu ni kuichezea timu hii na nampenda sana mchezaji Kipre Tchetche, namuiga anavyocheza na nataka kuwa kama yeye.”

Akizungumzia ujio wa wanafunzi hao, beki Said Morad, alianza kwa kumshukuru Mungu akisema kuwa ni faraja kubwa kupata ujio mkubwa kama huo huku akitoa wito kwa watu kuwekeza kwenye soka la vijana.

“Hivi ni vitu vinavyotambulika sana duniani, tumeona vikifanywa na Balotelli (Mario), Cristiano Ronaldo, wakifurahi na vijana pamoja, tumepata faraja kubwa sana siku ya leo,” alisema.

Uongozi wa Azam FC kupitia kwa mmoja wa wafanyakazi wa timu hiyo, ambaye ni Meneja wa Uwanja, Bi. Sikitu Kilakala, aliyeupokea ugeni huo sambamba na Keshia, Mwishehe Mchalo, alisema: “Tumefurahia sana ujio huu, tunaona jamii iko pamoja na sisi , inatukubali, sio hawa tu tunawakaribisha na wengine waje Azam FC, watu wengi wanasikia tu Chamazi lakiji hawajahi kufika, hivyo ni fursa kwao kuja hapa, Azam FC sio mpira peke yake bali hata mambo mengine ya kijamii tupo pamoja shughuli mbalimbali za kimichezo. Hata kauli mbiu yetu inaeleza vizuri ‘Timu Bora, Bidhaa Bora’.”