NYOTA wa Kimataifa wa timu ya Azam FC, Didier Kavumbagu, amesema kuwa wao kama washambuliaji wanatakiwa kufunga mabao mengi zaidi ili kutimiza lengo la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Mrundi huyo ameshaifungia mabao mawili Azam FC msimu huu ndani ya mechi mbili zilizopita, ambapo alifunga na kutegeneza bao wakati wakiichapa Toto Africans 5-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kavumbagu aliuambia mtandao huu mara baada ya mchezo huo kuwa ili kuweza kuwakimbia wapinzani wao Yanga wanapaswa kufunga mabao mengi kama walivyofanya dhidi ya Toto.

“Nafurahia mabao ninayoendelea kuyafunga, lakini kama kweli tunataka kuikimbia Yanga, sisi washambuliaji tunapaswa kufunga mabao mengi zaidi kama leo (jana),” alisema.

Nyota huyo aliyewahi kukipiga Yanga na Atletico ya Burundi, aliongeza kuwa: “Mabeki wamekuwa wakifanya kazi nzuri kuzuia tusifungwe, hivyo na sisi washambuliaji tunatakiwa kufunga mabao mengi ili kutimiza malengo tuliyojiwekea.”

Kavumbagu ndiye aliyekuwa kinara wa ufungaji bora kwa upande wa Azam FC msimu uliopita, akifunga mabao 10 na moja akifunga katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya El Merreikh katika mchezo wa kwanza ulioisha kwa Azam kushinda mabao 2-0 kabla ya kutolewa ugenini walipofungwa 3-0 dakika za mwisho.