NYOTA nane wa Azam FC, waliondoka jana asubuhi kuelekea Afrika Kusini, wakiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Stars imekwenda nchini humo kwa kambi ya siku 10 ikijiandaa na mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi dhidi ya Algeria ‘The Desert Foxes’ utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Novemba 14 mwaka huu.

Siku tatu baadaye watarudiana jijini Algiers, Algeria na mshindi wa jumla atafuzu kwa hatua ya makundi, ambayo itatoa timu tano za Afrika zitakazokata tiketi ya kushiriki michuano hiyo.

Wachezaji wa Azam FC, walioondoka ni kipa Aishi Manula, beki Shomari Kapombe, viungo Himid Mao ‘Ninja’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, winga Farid Maliki na nahodha John Bocco ‘Adebayor’

Nyota wengine wa Stars walioelekea huko ni makipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Said Mohamed ‘Nduda’, Juma Abdul, Ramadhan Kessy, Mohamed Hussein, Haji Mwinyi, Hassan Isihaka, Salim Mbonde, Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Pia Saimon Msuva, Salum Telela, Jonas Mkude, Said Ndemla, Ibrahim Hajibu, Malimi Busungu, huku mshambuliaji wa Stand United, Elias Maguli, akitarajiwa kuungana na kikosi hicho kesho baada ya kuitumikia timu yake katika  mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom leo dhidi ya Mgambo JKT na kuifungia bao pekee lililowapa ushindi.

Wakati Stars ikitarajia kurejea nchini Novemba 11, washambuliaji wake tegemeo Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa wanaocheza soka nje ya nchi, wataungana na timu hiyo mwishoni mwa wikiendi hii.