TIMU ya Azam FC jana mchana ilitembelea Kiwanda cha Bakhressa Food Products kilichopo Mwandege, Wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.

Msafara huo ulijumuisha timu yote ya wakubwa na vijana, makocha pamoja na uongozi wa timu hiyo.

Lengo kubwa la safari hiyo ilikuwa ni timu hiyo kufahamiana na wafanyakazi wa kiwanda hicho, ikizingatiwa taasisi zote mbili ni mali ya mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim Bakhressa.

Kiwanda hicho kinatengeneza baadhi ya vinywaji baridi vya aina ya Azam, vikiwemo Azam Cola, Orange, Fursana, Azam Embe, Pera, Azam Energy Drinks, Azam Malt, Maji ya Uhai.

Mkuu wa msafara huo, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alifurahia wao kufika kiwandani humo kwa kutembelea ndugu zao na kudai kuwa huo ni mwanzo tu kwani wamepanga kutembelea kampuni zote za Azam ili kufahamiana.

“Lengo kubwa ni kufahamiana na pia kutengeneza roho za watu kujua kuwa timu ni hii hapa na hii ni timu yetu na hatukukosea kwenye nembo yetu kuandika ‘Timu Bora, Bidhaa Bora’, kwa hiyo timu hii ni bora na bidhaa nazo ni bora, na tunachanganya vyote viwili ili kuweza kufika mbele zaidi,” alisema.

Kawemba alisema wanajisikia faraja kufika hapo na anaamini ya kuwa, daraja walilotengeneza baina ya pande zote mbili litawaletea mafanikio mengi zaidi.

Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Idrissa Nassor ‘Father’, ambaye pia ni Meneja Mauzo na Usafirishaji wa kiwanda hicho, alisema ana furaha kubwa kuzikutanisha pande zote mbili ambazo zilikuwa hazijuani.

“Mimi ninafuraha kama vile mtu anayejua ndugu wawili waliopoteana, halafu yeye anawajua, Azam FC mnajuana, Azam SSB wanajuana, lakini nyinyi wawili hamjuani na wote ni ndugu wa baba mmoja Azam, nyote wafanyakazi wa kampuni moja ya Azam, lakini hamjuani, kinachonifurahisha leo nimekutanisha ndugu wawili, nadhani kuanzia leo mtakuwa mmejuana,” alisema.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Gerhard Ungerer, alisema kuwa: “Baadhi yenu mmekuwa mkionja ladha ya bidhaa zetu, lakini hamjui namna zinavyotengenezwa, hapa tunatumia mashine bora za viwango vya dunia, teknolojia ni ya hali ya juu, ili kupata bidhaa bora tunatumia viungo bora kabisa vya dataja la juu duniani.”

“Karibuni sana mjisikie mpo nyumbani, nyinyi ni timu yetu, sisi tunajivunia kuwa nyinyi ni timu yetu na sio timu ya kimchezo mchezo bali ni timu thabiti, kwa hiyo nawatakia heri muendelee kazi nzuri na kuendelea kupeperusha vema bendera ya Bakhressa na Azam,” alisema Meneja Operesheni wa kiwanda hicho, Solomon Nzano.

Nzano pia alielezea historia fupi ya kiwanda hicho, akisema kilifunguliwa Mei 29, 2011 kikiwa na mashine tatu za hali ya juu kutoka Ujerumani, ambapo hivi sasa kimezidi kukua zaidi kwa kupanua biashara na bidhaa zinazozalishwa.

“Sisi tunazingatia sana ubora wa bidhaa zetu, katika wote walioajiriwa hapa, kuna watu wenye uzoefu mkubwa sana wengine wanatoka makampuni makubwa duniani wanaozalisha soda za ushindani kama hizi, kwa hiyo ujuzi walioleta ni mkubwa sana kiasi kwamba ile soda au juisi inayozalishwa kwenye hiki kiwanda inaweza kushindana na bidhaa yoyote ulimwenguni na kushinda nishani,” alisema.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Allan Wanga, alipewa fursa kuzungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake na kusema kwa ufupi kuwa wamefurahishwa na safari hiyo na akawapongeza walioandaa na kudai itawafunza mengi waliyokuwa hawayajui.