TIMU ya Azam FC kesho inatarajia kuivaa Toto Africans mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, imepania kushinda na kuendelea kutawala kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Kabla ya mchezo wa Yanga wa jioni hii dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC ndio ipo kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 22 ikiwazidi pointi mbili wanajangwani hao.

Azam FC imefikisha pointi hizo baada ya kushinda mechi saba na sare moja, wapinzani wao Toto Africans mpaka sasa wamejikusanyia jumla ya pointi 13 katika nafasi ya nane wakiwa wameshinda mechi tatu, sare nne na vipigo viwili.

Hadi zinaingia katika mchezo huo, Azam FC imetoka kuifunga JKT Ruvu mabao 4-2 kwenye mchezo uliopita huku Toto Africans nayo ikiichapa Mgambo JKT bao 1-0.

Azam FC ina nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo hasa kutokana na rekodi mbaya waliyokuwa nayo Toto Africans katika mechi za ugenini, mpaka sasa wameambulia pointi tatu tu ugenini kwenye michezo minne ya ugenini waliyocheza.  

Pia rekodi ya Azam FC kutofungwa mpaka sasa kwenye mchezo wowote wa nyumbani na ugenini ni moja ya vikwazo vitakavyoipa ugumu timu hiyo, iliyopanda daraja msimu huu.

Rekodi inaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 10 kwenye mechi za ligi kabla Toto haijashuka daraja mwaka juzi na kupanda tena mwaka huu, Azam FC imeshinda tano na Toto Africans mara mbili huku michezo mitatu wakienda sare.

Makali ya safu ya ushambuliaji ya Azam FC chini ya kinara wa mabao ndani ya timu hiyo msimu huu, Kipre Tchetche, aliyefunga matano mpaka sasa na nahodha John Bocco aliyeingia wavuni mara tatu, nayo inatarajia kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Toto kama safu yao ya ulinzi haitajipanga vema.

Akizungumza na mtandao huu kuhusu mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, alisema watapambana zaidi kwenye mchezo huo kuhakikisha wanashinda ili waendelee kukaa kileleni.

“Ligi ni michezo 30, hivi sasa sisi tupo juu baada ya kucheza mechi nane, hivyo bado tuna jitihada kubwa tunatakiwa kuzifanya, kukaa kileleni kunatupa matumaini ya kutwaa ubingwa na hata wachezaji inawapa moyo,” alisema.

Kitambi aliongeza kuwa kutokana na timu hiyo kucheza mechi mbili ndani ya siku nne, wataangalia ni namna gani ya kukabiliana na uchovu wa wachezaji kuelekea mchezo huo.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, ikishinda mchezo huo itafikisha jumla ya pointi 25 na kuendelea kukaa kileleni hadi pale ligi itakapoendelea tena baada ya mapumziko mafupi ya ligi kupisha mechi za timu za Taifa, michuano ya Kombe la Chalenji, Mapinduzi na usajili wa dirisha dogo.