UONGOZI wa timu ya Azam FC umesikitishwa na kauli ya mshambuliaji wao, Didier Kavumbagu, aliyoitoa kwenye vyombo vya habari, akidai kuwa ataondoka ndani ya timu hiyo kwenye dirisha dogo kama akiendelea kuwekwa benchi.

Kavumbagu alitoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya JKT Ruvu uliofanyika Uwanja wa Karume juzi na kuisha kwa Azam FC kushinda mabao 4-2, huku nyota huyo wa Burundi akifunga bao la kwanza.

Akizungumza na mtandao huu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema hakuna shinikizo lolote kutoka kwao uongozi juu ya upangaji wa kikosi, bali ni falsafa ya Kocha Mkuu Stewart Hall, anayependa kutumia wachezaji waliokuwa fiti kwa ajili ya kuipatia timu ushindi.

“Ni utaratibu wa mwalimu wetu, anacheza wachezaji kwa kufanya mabadiliko, ukiangalia timu yetu kwa sasa inao washambuliaji watano, tunaye Allan Wanga, John Bocco, Kipre Tchetche, tunaye Kavumbagu mwenyewe na Ame Ally, kwa kila mchezo mwalimu huwa anachagua washambuliaji watatu walio fiti.

“Inawezekana akajiona kuwa hakupata nafasi ya kucheza, lakini lazima ajue ameweza kushiriki kwenye michuano ya Kombe la Kagame na sasa hivi kwenye ligi amecheza katika mechi tatu hadi kufikia sasa raundi ya nane, na ameweza kucheza vizuri sana katika mchezo wa mwisho na hii ndio faida ya kucheza ukiwa upo fiti,” alisema.

Kawemba alimtaka Kavumbagu kupambana na kuweza kuwania namba na wenzake huku akidai kuwa hata kwenye eneo la kiungo wamekuwa na viungo saba na kocha amekuwa akitumia falsafa ile ile ya kuwabadilisha kulingana na aina ya mchezo.

“Kocha anasema sehemu muhimu kwenye timu yake ni kiungo na ushambuliaji, hivyo anapanga wachezaji waliokuwa fiti asilimia 100 ili kupata ushindi, huo ndio mfumo wa mwalimu.

“Hivyo kama kuna mchezaji anaona ana nafasi finyu kwenye timu, Azam utaratibu ni mmoja tu, mchezaji yoyote ambaye anaona hana nafasi na hataki kuendelea kuwepo kwenye timu, mwalimu huwa hawezi kumshikilia na yeye ndiye anafanya usajili kwenye timu,” alisema.

Bosi huyo aliongeza kuwa: “Kwa sasa tunaamini ya kuwa safu ya ushambuliaji ipo sawa sawa, wakati wowote ukimtoa mtu na kumuingiza mtu, timu inakuwa bado inacheza vizuri, mshambuliaji yoyote anayeingizwa hata zikiwa zimebakia dakika 30, bado amekuwa akifanya vizuri, mfano Kipre Tchetche amefanya hivyo kila alipoingizwa.”

Kavumbagu ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa Azam FC msimu uliopita akifunga mabao 10, aliuanza msimu huo kwa kasi, lakini raundi ya pili akashindwa kufanya vizuri.