TIMU ya Azam FC kesho inaweza kukaa kileleni kwa mara ya kwanza kwenye msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kama itaichapa JKT Ruvu katika mechi ya ligi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Azam FC ikishinda itakuwa imefikisha jumla ya pointi 22 na kuishusha kileleni Yanga iliyofikisha pointi 20 leo mara baada ya kuambulia sare ya mabao 2-2 walipocheza na Mwadui kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Tayari Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, amesema mchezo huo utakuwa mgumu huku akitabiri upinzani mkubwa kutoka kwa mshambuliaji wao wa zamani, Gaudence Mwaikimba, aliyehamia JKT Ruvu msimu huu.

Hall pia amesema kuwa Uwanja wa Karume nao hauko vizuri, hasa ardhi yake ya kuchezea na kudai kuwa watacheza wakiwa na lengo la kuendeleza matokeo yao mazuri waliyopata.

Kutokana na matokeo mabaya ya JKT Ruvu waliyokuwa nayo, wakiwa wameambulia sare mbili na vipigo sita mpaka sasa, Nahodha wa Azam FC, John Bocco, amesema kuwa hilo halitawafanya  waidharau timu hiyo.

“Sisi hatuidharau timu yoyote kwenye ligi kwa sababu timu zote zinajiandaa vizuri, naamini kila timu inataka kupigania ubingwa na ukiangalia ligi ipo mwanzoni, kwa hiyo wamepoteza mechi zilizopita, naamini wanapigana kupata matokeo mechi ijayo (kesho).

“Mechi itakuwa ngumu, ukiangalia JKT ni timu kubwa na sio mbaya, hivyo mchezo utakuwa mzuri na mgumu kwa upande wetu, lakini tumejipanga kushinda,” alisema Bocco.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu msimu wa 2013/14, wataingia dimbani wakiwa na kumbukumbu ya kushinda ugenini bao 1-0 kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ndanda FC, huku JKT Ruvu ikiambulia suluhu walipochuana na Mtibwa Sugar.

Kikosi cha Azam FC kitaimarika kwenye mchezo huo kwa kuwatumia nyota wake kipa Aishi Manula, winga Farid Maliki na viungo Michael Balou na Mudathir Yahya, walioukosa mchezo uliopita kutokana na majeraha madogo yaliyokuwa yakiwasumbua.

Vilevile kiungo mbunifu Salum Abubakar ‘Sure Boy’, naye atarejea kikosini baada ya kuukosa mchezo uliopita alipokuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi moja kutokana kukusanya kadi tatu za njano mfululizo.

Kocha Hall naye atarejea kwenye benchi la ufundi baada ya kutoruhusiwa kukaa katika mechi mbili zilizopita kutokana na kutolewa nje na mwamuzi wakati wa mchezo dhidi ya Coastal Union, ulioisha kwa Azam Fc kushinda mabao 2-0.

JKT Ruvu ambayo inaburuta mkia kwenye ligi hiyo, imefanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi, ambapo kocha mpya Abdallah Kibadeni ‘King’, atakuwa akiiongoza timu hiyo kwenye mechi yake ya tatu tokea alipochukua mikoba hiyo akimrithi Fred Felix Minziro.

Kihistoria tokea Azam FC ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2008/09, imekutana na JKT Ruvu mara 14 kwenye ligi, Azam ndio inaongoza kushinda mechi nyingi ikiwa imeibuka kidedea mara saba, JKT Ruvu nayo imeshinda nne huku michezo mitatu ikienda sare.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, mpaka sasa imecheza jumla ya mechi saba msimu huu ikiwa haijapoteza mchezo wowote kama Yanga, ikishinda sita na kutoa sare mchezo mmoja.