KOCHA Mkuu wa timu ya Azam, Stewart Hall, amesema kuwa wanatarajia upinzani mkali kutoka kwa mshambuliaji wao wa zamani, Gaudence Mwaikimba, watakapoivaa timu yake mpya ya JKT Ruvu Alhamisi ijayo kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mwaikimba ataikamia Azam FC kutokana na mshambuliji huyo kuwahi kukipiga katika timu hiyo kwa misimu mitatu kabla kuondoka msimu huu baada ya mkataba wake kuisha.

“JKT ina wachezaji wa Azam, kama vile Mwaikimba atakayepambana vikali kutuonyesha kuwa bado yumo na ana mapenzi na Azam FC, hivyo itakuwa ni mechi ngumu,” alisema Hall alipozungumza na mtandao huu.

“Mechi itakuwa ngumu kiukweli, pia Uwanja wa Karume wa nyasi bandia hauko kwenye ubora wake, hasa ardhi yake ikiwa siyo nzuri.”

Mwingereza huyo aliongeza kuwa, mpaka sasa kikosi chake kipo safi, hasa ikizingatiwa wachezaji waliokuwa na majeraha madogo, Farid Maliki, Michael Balou, Aishi Manula, walioukosa mchezo uliopita dhidi ya Ndanda kuanza mazoezi kwa ajili ya kuivaa JKT Ruvu.

Azam imeanza leo saa 9 alasiri mazoezi yake ya kujiandaa na mchezo huo.

Wakati Azam FC ikishika nafasi ya pili kwa pointi 19 kwenye msimamo wa ligi sawa na vinara Yanga, JKT Ruvu yenyewe inapumulia mashine kutokana na kujikusanyia jumla ya pointi mbili tu mpaka sasa katika mechi nane, huku ikiwa haijashinda mchezo hata mmoja.