Kocha Mkuu wa timu ya Azam FC, Stewart Hall, amesifia mazoezi ya ufukweni waliyofanya leo asubuhi kwenye fukwe za bahari ya Coco Beach, akidai yanawapa uimara wachezaji wake.

“Ni mazuri sana kwa misuli, unaweza kufanya kazi au kitu ufukweni, ambayo huwezi kuifanya kwenye ardhi ya kawaida. Yanatupa uimara katika enka na viungo kwa sababu mchanga unahama dhidi yako.

“Hivyo yanaongeza uimara, pia tunafanya mazoezi ya kibaolojia kwa sababu mchanga ni laini unaofanya mazoezi kuwa magumu, lakini mepesi kwa viungo…Mazoezi ni magumu lakini uzito wa viungo ni mdogo kutokana na mchanga,” alisema Hall.

Hall aliongeza kuwa kuna faida nyingi sana za kufanya mazoezi kwenye mchanga na amekuwa akiwaandalia programu hiyo wachezaji wake angalau mara moja kwa wiki mbili.

Katika mazoezi hayo, Hall aliongozana na wasaidizi wake Mario Marinica, Dennis Kitambi, Kocha wa Makipa Idd Abubakar na wa viungo, Adrian Dobre.

Wachezaji waliokuwa na majeraha madogo na kuukosa mchezo uiliopita dhidi ya Ndanda ulioisha kwa Azam FC kushinda bao 1-0, Michael Balou, Farid Maliki, Aishi Manula, wote walifanya mazoezi ya nguvu ufukweni na kudhihirisha kuwa wapo fiti. 

Kikosi cha Azam FC kilifanya mazoezi hayo kwa takribani saa 1.30 tokea saa 2 asubuhi leo, ambapo yalipomalizika wachezaji wote waliruhusiwa kwenda kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Taifa kesho.

Wachezaji wote wataripoti tena kambini keshokutwa na kufanya mazoezi mazoezi yao saa 9.00 alasiri keshokutwa kwa ajili ya kujiandaa na mchezo dhidi ya JKT Ruvu utakaofanyika Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam.

Matajiri hao wa Azam Complex, wanaodhaminiwa na Benki ya NMB wanashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 19 sawa na vinara Yanga inayoongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.