JUMLA ya mashabiki 100 wa timu ya Azam FC wanatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kesho alfajiri kuelekea mkoani Mtwara ili kuipa sapoti timu hiyo itakapocheza mchezo wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona saa 10 jioni siku hiyo.

 

Akizungumza na mtandao huu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, alisema mashabiki hao kwenda mkoani humo ni moja mikakati yao kama uongozi kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

 

“Sisi kama uongozi tumejipanga vilivyo kwenye mchezo huo, kama unavyoona timu imeondoka mapema kuelekea Mtwara, imefikia kwenye hoteli bora na sasa ujio wa mashabiki hao ni sehemu ya kutimiza lengo hilo, kwani wachezaji watapata sapoti kubwa,” alisema.

 

Aliongeza kuwa mashabiki 50 watapanda basi kubwa jingine la Azam FC, huku waliobakia  wakipanda mabasi ya kukodi, wote wakiondoka alfajiri ili kuiwahi mechi hiyo.

 

Kihistoria timu hizo zimecheza mechi mbili za ligi zote zikiwa ni msimu uliopita, Ndanda ilishinda nyumbani bao 1-0 kabla ya Azam FC kupata ushindi kama huo kwenye Uwanja wa Azam Complex ziliporudiana bao lililofungwa na Gaudence Mwaikimba, aliyehamia JKT Ruvu msimu huu.

 

Lakini kabla ya kuanza msimu huu, Azam FC iliyokuwa na kikosi mchanganyiko cha timu ya vijana na baadhi wakubwa, ilicheza mechi maalumu ya kuadhimisha Ndanda Day katika Uwanja wa Nangwanda Agosti 29 mwaka huu iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.

 

Hiyo itakuwa ni mechi ya tatu ya ugenini ya Azam FC msimu huu, mbili zilizotangulia ilicheza mkoani Shinyanga na kuzifunga Stand United mabao 2-0 na Mwadui bao 1-0.

 

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB, mpaka sasa imejikusanyia pointi 16 kwenye mechi sita ilizocheza, ikishinda tano na  sare moja dhidi ya Yanga (1-1) kwenye mchezo uliopita.